Bayern Munich, Madrid kisasi Ligi Mabingwa Ulaya

Muktasari:

  • Real Madrid itakuwa ugenini kumenyana na Bayern Munich katika mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya utakaochezwa kwenye Uwanja wa Allianz Arena.

Munich, Ujerumani. Cristiano Ronaldo ametua katika ardhi ya Ujerumani akiwa ameongoza nyota wa Real Madrid kwa mchezo wa leo dhidi ya Bayern Munich.

Real Madrid itakuwa ugenini kumenyana na Bayern Munich katika mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya utakaochezwa kwenye Uwanja wa Allianz Arena.

Timu za Ujerumani imekuwa ikiteswa na timu za Hispania katika miaka ya hivi karibuni baada ya kutupwa nje kwenye kwa misimu minne mfululizo.

Bayern Munich iliondolewa na Real Madrid mwaka 2014 na mwaka jana timu hiyo iling’olewa tena katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kocha wa Real Madrid Mfaransa Zinedine Zidane ana matumaini ya kupata matokeo mazuri katika mchezo huo.

Mbali na Zidane, Rais wa Real Madrid Florentino Perez alikuwa miongoni mwa vigogo waliopanda ndege kwenda Ujerumani.

Baadhi ya wachezaji nyota wa Real Madrid akiwemo Ronaldo, Casemiro, Marcelo na kipa namba moja, Keylor Navas walikuwa na nyuso za matumaini ya kupata matokeo mazuri.

Zidane alisema mshambuliaji nguli Karim Benzema amerejea kwenye kiwango bora na huenda akacheza mchezo huo unaotarajiwa kuwa mkali. “Nimemuona katika mazoezi anafanya vyema, anafunga mabao. Anafanya kazi nzuri akili yake ipo katika mchezo ujao,” alisema Zidane.

Benzema, nyota wa kimataifa wa Ufaransa, amefunga mabao tisa katika michezo 39 aliyocheza msimu huu katika kikosi cha Zidane.

Wakati Real Madrid ikionekana kupania mchezo huo, mshambuliaji Robert Lewandowski aliwaongoza nyota wa Bayern Munich katika mazoezi ya mwisho.

Lewandowski, ambaye amekuwa akihusishwa na mpango wa kujiunga na Real Madrid, alifanya mazoezi kwa kiwango bora. Pia Arjen Robben na James Rodriguez wanatarajiwa kuikabili timu yao ya zamani Real Madrid katika mchezo huo.