Baba ampeleka Kun Aguero Barcelona

Muktasari:

Msimu wa fowadi huyo wa kimataifa wa Argentina umeshafika tamati baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti wiki, licha ya kuwapo na uhakika mkubwa kwamba anaweza kuwa fiti kwenda kukipiga kwenye fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika Russia kuanzia Juni mwaka huu.

BARCELONA, MADRID

BABA mzazi wa straika wa Manchester City, Sergio Aguero amesema inawezekana kabisa kwa mwanaye kwenda kujiunga na Barcelona ya Hispania.

Msimu wa fowadi huyo wa kimataifa wa Argentina umeshafika tamati baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti wiki, licha ya kuwapo na uhakika mkubwa kwamba anaweza kuwa fiti kwenda kukipiga kwenye fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika Russia kuanzia Juni mwaka huu.

Baba wa mchezaji huyo, Leonel del Castillo alifichua hatima ya mtoto wake na kubainisha kile kinachoweza kufanyika katika dirisha lijalo la usajili.

Alipoulizwa kama mwanasoka huyo atarudi kwenye klabu ya Independiente, Leonel alisema: “Kila ninapomuuliza, Sergio amekuwa akiniambia kwamba atarudi Independiente lakini hakusema ni lini.”

Leonel aliulizwa pia kama anaona uwezekano wowote wa mwanaye kwenda kucheza timu moja na staa mwenzake wa Argentina, Lionel Messi huko Barcelona, alisema: “Inawezekana, msimu ujao wachezaji kibao watabadili timu zao...”