HIVI karibuni Mbrazili Marcio Maximo amemaliza mkataba wake wa kipindi cha miaka minne cha kuinoa Taifa Stars, huku mafanikio pekee yakiwa ni kuipeleka timu hiyo kwenye michuano ya kwanza ya Mataifa ya Afrika inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN).
Mbrazili huyo alipofika matarajio ya wengi yalikuwa makubwa lakini pia wapo waliokuwa na maoni wasiwasi.
Kuna watu waliamini bado tulikuwa na safari ndefu ya kufika huko tunakotakiwa.
Sasa kitu cha kusikitisha Maximo hakufanikiwa kutupeleka kwenye mashindano makubwa kama yale ya Mataifa ya Afrika (CAN) au kwenye Kombe la Dunia.
Nilikuwa ni kati ya wale wachache waliokuwa na fikra za kwamba bado tulikuwa tunatakiwa kufanya mambo makubwa zaidi ili kufika mbali.
Fikra yangu kubwa ilikuwa kuandaliwa na programu ya muda mrefu, ambayo ingetufikisha kwenye mafanikio.
Bahati mbaya wakati wa ujio wa Marcio Maximo, sikuwahi kuiona programu yake.
Kitaifa malengo yalikuwapo kwa mfano kufuzu kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 2008 na zile za mwaka huu nchini Angola.
Kama tungefanikiwa kufuzu kule Ghana tungekuwa na bahati kubwa kwani bado hatukuwa na kiwango hicho cha kufika hatua hiyo.
Hali kadhalika miaka miwili iliyofuata tuliposhindwa kwenda Angola kusema kweli bado hatukuwa tumejiandaa vya kutosha kuelekea huko.
Kwa mara nyingine naliangalia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kama limejipanga vipi na kocha mpya, Jan Poulsen kutoka Denmark.
Hapa nikizungumzia programu yake ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu, ambazo Watanzania hawakuwekewa wazi na kocha aliyepita, hali iliyowafanya kuwa na matarajio makubwa kupitiliza.
Watanzania tuna wasiwasi hasa kuelekea michuano ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka 2012, na mtihani wa kwanza ukiwa Septemba dhidi ya Algeria.Kocha mpya ana mtihani mzito kwani atakuta Watanzania wamechoshwa mno na kufanya vibaya.
Ikumbukwe mara ya mwisho kwa Stars kutinga kwenye Fainali za Kombe la Mataifa (CAN) ilikuwa mwaka 1980.
Kuendelea kuboronga kwa Stars kutakimbiza wadhamini na ndio maana TFF inatakiwa kuwa makini katika suala zima la kuiandaa Stars.
Ni imani yangu kwamba, kocha huyo mpya atatambua ni nini Tanzania inachotaka, na nini inachokosa, na kitu ambacho kocha aliyepita amekiacha kinachohitaji kuendelezwa.
Kwa mfano Maximo alipokuwepo nchini alitakiwa kuendesha kozi mbalimbali ili kuzalisha makocha wa kutosha, lakini hilo halikufanyika.
Tunasubiri kuona Poulsen naye atakuja na mipango ipi, ambayo itatutoa kimasomaso Watanzania.