OLIVER ALBERT
BEKI wa kushoto John Njoroge amesema amegoma kuuzwa Serbia ndio maana Kosta Papic akamfukuza Yanga, lakini kocha huyo wa Serbia amesema Mkenya huyo ni mtovu wa nidhamu.
Papic alimtimua Njoroge katikati ya wiki iliyopita kwenye mazoezi ya Yanga kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kwa madai ni mkaidi.
Njoroge amepasua bomu na kusema: "Tatizo lilianza baada ya kuniambia anataka kunipeleka Serbia, nikamwambia sitaki kwenda huko bora nirudi kwetu, hapo ndipo utata ulipoanza."
"Alianza kunitafutia sababu, lakini huwezi kunilazimisha kwenda sehemu ambayo siipendi, nimechoshwa na huu mpira wa Tanzania, hapa naisubiri TFF ndio wataamua, kwanza ameniharibia hata katika timu ya taifa ya Kenya."
Njoroge akizungumzia majibizano yaliyotokea baina yao mazoezini alisema: "Siku ile mazoezini aliniambia mimi na yeye yamekwisha, nikamuuliza kwa vipi wakati nimesainia mkataba, akasisitiza yamekwisha na ndio maana nikawa najibizana naye, hakunitendea haki."
"Nilimaliza mkataba msimu uliopita, mwenyewe alinitafuta sana kwa simu hadi akatuma watu nikakubali nikaongeza mkataba wa mwaka mmoja sasa wakati niko Kenya likizo, alikuwa na tiketi yangu akanicheleweshea kusudi halafu ananilaumu kuwa nimechelewa mazoezini, lengo lake anataka kunifuza.
"Kama aliona amesajili wachezaji wengine na hanihitaji, angeniambia mapema nikiwa Kenya sasa ameniharibia mipango yangu, nitacheza timu gani na usajili unaelekea ukingoni, kuna timu nyingi zilikuwa zikinihitaji lakini nikaachana nazo nije kucheza Yanga."
Papic alipoulizwa na Mwanaspoti alisema tatizo ni Njoroge mwenyewe kuchelewa kuripoti mazoezini mpaka tarehe ya usajili ikapita.
"Alitumiwa tiketi mapema kabisa, lakini hakuja, imefika tarehe ya mwisho ya usajili hakuwapo, nisingemsajili mtu ambaye sina uhakika naye, kwa hiyo nikawapa nafasi wachezaji ambao wapo," alisema Papic.
"Amekuja mazoezini nikamwambia kuwa amechelewa usajili, akaniambia kwanini sikumwambia mapema ili aende Simba au Sofapaka, nikamjibu ningemwambia wapi wakati hakuwapo nchini. Ili kumsaidia nilimwambia kuwa kama anataka nimpeleke Serbia, lakini aligoma."