MICHAEL MOMBURI
MADAKTARI wamemwambia mshambuliaji wa Simba, Emanuel Okwi atulie nje ya uwanja kwa muda wa siku saba bila kugusa mazoezi ya kocha wa muda Syllersaid Mziray.
Okwi ambaye ni raia wa Uganda alirejea nchini wiki iliyopita lakini baada ya kufanya mazoezi siku moja akatonesha nyonga ambayo aliumia akiwa likizo kwao.
"Niliumia mazoezini nilipokuwa Uganda nikadhani nimepona, nilipokuja kuanza mazoezi Simba nikatonesha ndio maana imebidi nibaki Dar es Salaam kwa matibabu,"alieleza mchezaji huyo wa zamani wa SC Villa.
"Madaktari wameniambia nitakaa nje ya mazoezi kwa wiki moja kwa hiyo inamaana wikiendi ijayo nitakuwa tayari kujiunga na wenzangu kambini Zanzibar. Naendelea vizuri sana wala hakuna haja ya mashabiki kuwa na wasiwasi."
"Hili tatizo ni la kawaida kwa wachezaji wengi, lakini maandalizi nimeona yanaendelea vizuri ndani ya Simba,"alisisitiza mchezaji huyo ambaye licha ya Simba kushindwa kufurukuta Kombe la Kagame msimu uliopita aliacha jina jijini Kigali kwa kazi yake.
Simba inaendelea na mazoezi makali Zanzibar chini ya Mziray baada ya Kocha Mkuu Patrick Phiri kususa kurejea huku uongozi ukisisitiza kumsimamisha. Wachezaji wengine ambao hawapo kambini Zanzibar kwasababu mbalimbali ni Patrick Ochan, Joseph Owino, Mbwana Samatta na Kelvin Chale.