MWANDISHI WETU
YANGA inatakiwa kuwa makini kwani kocha wake Kosta Papic ametajwa na baadhi ya klabu za Afrika Kusini katika orodha ya makocha wanaotakiwa sasa.
Papic, ambaye amewahi kufundisha katika klabu tatu za Afrika Kusini yumo katika orodha ya Moroka Swallows na Platinum Stars ili kuziimarisha katika msimu ujao wa Ligi Kuu Afrika Kusini
Ingawa, Papic mwenyewe amesema hana taarifa hizo, lakini baadhi ya vyombo vya habari vya Afrika Kusini vimekuwa vikimtaja Papic kuwa ni miongoni mwa makocha wanaowindwa na klabu kadhaa za Sauzi zikiwamo; Moroka na Platinum.
Mashabiki wa Afrika Kusini wamekuwa wakimpa sifa nyingi Papic na wamekuwa hawaelewi sababu ambazo zilimfanya akaondoka nchini humo.
Papic ndiye kocha pekee katika historia ya Afrika Kusini kufundisha timu mbili pinzani, Orlando Pirates na Kaizer Chiefs kwa vipindi viwili tofauti ingawa aliwahi kuikochi pia Mertizburg.
Mashabiki kadhaa wa Afrika Kusini waliiambia Mwanaspoti wakati wa fainali za Kombe la Dunia kuwa Papic ni kocha mzuri, lakini alikuwa na balaa na kukutana na viongozi wabinafsi wa Orlando Pirates na Kaizer Chiefs.
Papic alipoulizwa kama yupo tayari kurudi Afrika Kusini alisema: "Nina mkataba na Yanga, bado sijaambiwa lolote, ila kama wakija tutajadiliana."
Tangu atue nchini Oktoba mwaka jana, Papic ameibadilisha Yanga na kuifanya icheze soka ya burudani na kuvutia tofauti na miaka mingine ya nyuma.