OLIVER ALBERT
RAZAK Khalfan amesema anaendelea vizuri na majaribio kwenye timu ya Seattle Sounders FC inayoshiriki Ligi Kuu Marekani lakini amedokeza akishindwa atatimkia Canada.
Razak, ambaye ni mdogo wa kiungo wa timu ya Taifa ya Tanzania, Nizar Khalfan anayechezea Vancouver Whitecaps ya Canada aliiambia Mwanaspoti kutoka Marekani kuwa atahakikisha anakabiliana na ushindani uliopo katika timu hiyo ili asajiliwe.
"Sasa nipo Sounders nafanya majaribio ila mambo yakiwa mabaya hapa nitakwenda Canada kusaka timu nyingine," alisema Razak, ambaye ni mchezaji wa Yanga.
Razak alisema vita ya namba lakini atahakikisha anapigana kufa na kupona ili asajiliwe.
Kiungo huyo akifanikiwa kuchezea timu hiyo atakuwa Mtanzania wa pili kucheza Ligi Kuu ya Marekani baada ya Sunday Manara kwenye miaka ya 1970.