Vitimbwi nilivyokutana navyo Kombe la Dunia Afrika Kusini
Patrick Viera wa Man City na Mhariri wa Mwanaspoti Frank Sanga kwenye uwanja wa Loftus Versfeld mjini Pretoria.
Frank Sanga
NI saa nne asubuhi Jumatano ya Juni 9, nimefika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa O.R Tambo jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Mambo yamechangamka, mashabiki wengi wa soka wa Mexico, Slovakia, Hondurus na Argentina nao wametua muda huo, wanapiga picha katika makundi. Ninatoa kamera yangu na kuwapiga picha, wanashangilia.
Ninaachana na mashabiki hao na kwenda kwenye hoteli ambayo nimefikia maeneo ya Kempton Park. Nikiwa naelekea kwenye hoteli hiyo nashuhudia shamrashamra, watu wamevaa jezi za Bafana Bafana, mavuvuzela yanauzwa kwa wingi mitaani, magari yamepambwa kwa bendera ya Afrika Kusini. Inavutia na kupendeza.
Baada ya kukaa saa moja hotelini, nakwenda makao makuu ya muda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) yaliyopo jengo la Mandela Square, Sandton. Kabla ya kufika huko barabarani nakutana na utitiri wa mashabiki wa soka ambao wamejipanga barabarani wakitaka kuwaona wachezaji wa Bafana Bafana ambao wamebebwa katika mabasi matatu yanayopita mitaa mbalimbali ya Johannesburg huku fainali zikitarajia kuanza siku tatu baadaye.
Ninapiga picha nyingi za maandamano hayo, na ninakwenda zangu makao makuu ya Fifa kuchukua kitambulisho changu kwa ajili ya kuingia uwanjani na kuripoti mechi mbalimbali za Kombe la Dunia. Sandton napo hapafai, watu wamejazana kutoka kila pembe ya dunia.
Baada ya kujitambulisha naambiwa kuwa vitambulisho kwa waandishi wa habari vinatolewa kwenye viwanja, hivyo nashauriwa niende Ellis Park au Soccer City. Ni tayari jioni sana, maandandamo ni makubwa, siwezi kuwahi katika viwanja hivyo. Narudi hotelini ili asubuhi nishughulikie kitambulisho.
Siku ya pili, ambayo ni Alhamisi ninakwenda moja kwa moja kwenye Uwanja wa Ellis Park, naingia kwenye kituo cha utoaji wa vitambulisho (Accreditation Centre) ambako nakutana na msururu wa waandishi wa habari kutoka duniani kote wakisuburi vitambulisho vyao. Kila mwandishi alitakiwa kutuma maombi ya kupata vitambulisho vya fainali hizo kabla ya Januari 30 mwaka huu na ndivyo nilivyofanya. na inapofika zamu yangu napata kitambulisho na ninaelekezwa kuchagua mechi moja kila siku kwani kila mwandishi anatakiwa kuchagua mechi moja kwa siku ili apewe tiketi ya kiti cha kukaa katika kila mechi. Kila tiketi hutolewa siku ya mechi kwenye chumba cha habari cha uwanja husika.
Baada ya kupewa kitambulisho hicho kazi inakuwa rahisi, lakini bado kuna tatizo kubwa moja; baridi, baridi, baridi.
Mechi ya kwanza kati ya Bafana Bafana dhidi ya Mexico katika Uwanja wa Soccer City Ijumaa ya Juni 11, ninaingia uwanjani nikiwa nimevaa mavazi ya kawaida, ingawa kuna baridi naona ni hali ya kawaida kwa sababu pengine ya furaha ya kuangalia mechi ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.
Siku inayofuata ninakwenda kwenye Uwanja wa Ellis Park kuangalia mechi baina ya Argentina na Nigeria. Ninatamani mpira uishe mara moja nirudi hotelini, sina hamu kwa sababu baridi kali. Televisheni kubwa mbili za uwanjani zinatoa maandishi; "It is Cold, Feel It'. Ninaandika kila tukio ambalo linaendelea uwanjani humo, huku mikono yangu ikitetemeka kwa baridi kali. Hii si baridi ila ni barafu.
Mechi inapoisha ninakimbia haraka kwenye chumba cha mkutano wa waandishi wa habari. Baada ya kumaliza mkutano huo, naandika habari haraka haraka na kuituma gazeti la Mwananchi, huku nikikimbilia katika basi ambalo ni maalumu kwa waandishi wanaoishi maeneo ya Kempton Park na Uwanja wa Ndege wa O.R Tambo.
Siku inayofuata ni Jumapili, ninakwenda kwenye maduka ya Eastgate kutafuta makoti na nguo za joto, na baada ya kujiweka sawa, ninakwenda kituo cha mabasi ili niwahi mechi ya Algeria na Slovania ambayo inafanyika kwenye Uwanja wa Peter Mokaba mjini Polokwane. Ni mwendo wa saa nne kutoka Johannesburg mpaka Polokwane. Mechi ni ya mchana hivyo nafanya haraka ili niwahi.
Ninapofika Polokwane saa sita mchana, nakwenda moja kwa moja kwenye chumba cha habari cha uwanja huo na kuchukua tiketi yangu na moja kwa moja naingia uwanjani kuona mechi hiyo ambayo inaanza saa 7:30 mchana.
Saa 10:00 jioni nimemaliza shughuli zangu zote ikiwa ni pamoja na kutuma habari Mwananchi kuhusu mechi hiyo, kabla ya kupanda basi na kurejea Johannesburg ambako ninafika saa nne usiku.
Kuanzia hapo ninakuwa na ratiba ngumu kwani ninatakiwa kusafiri karibu kila siku kutokana na mechi za Kombe la Dunia kufanyika katika viwanja kumi tofauti ambavyo vipo mbali kutoka ninapoishi Johannesburg.
Siwezi kusahau nilipokwenda kwenye mechi ya usiku kati ya Mexico na Ufaransa mjini Polokwane Juni 17, kwani baada ya mechi kwisha saa nne na nusu usiku, nilijikuta nikikosa usafiri wa kurejea Johannesburg mpaka saa nane usiku nilipopata usafiri wa mabasi yanayotoka Harare, Zimbabwe na nikafika Johannesburg saa moja asubuhi huku nikitakiwa kwenda kwenye mazoezi ya Denmark asubuhi hiyo na kuhudhuria mkutano saa tano kwenye Uwanja wa Soccer City. Ilikuwa ni kukimbia kila wakati kwa siku zote.
Ilikuwa lazima niende mazoezi ya Denmark kwa sababu nilitaka kukutana na beki Mtanzania, Patrick Mtiliga ambaye mama yake ni raia wa Denmark. Siku hiyo ni kocha tu aliyezungumza na waandishi wa habari, wachezaji hawakuruhusiwa. Nashukuru kwamba nilimpata Mtiliga baada ya mechi ya Denmark dhidi ya Uholanzi.
Ilikuwa ni ratiba ngumu sana kwangu, kwa sababu kila asubuhi nilitakiwa kuwa katika mazoezi ya timu ambayo imepangwa maalumu kwa waandishi wa habari siku hiyo, kila saa tano asubuhi kulikuwa na mkutano wa waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Soccer City, lakini pia kulikuwa na mikutano ya mara kwa mara ya Fifa kwenye Ukumbi wa Sandton, mikutano ya polisi na taasisi mbalimbali.
Siku zote ambazo zina mechi katika viwanja vya Ellis Park na Soccer City nilijikuta nikirejea hotelini saa sita usiku, lakini kwa viwanja vya mbali ilikuwa narejea siku inayofuata asubuhi huku usiku wote nikiwa safarini. Ilichosha na hasa kutokana na baridi kali ya usiku.
Jambo ambalo nililipenda ni kuona Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga akiwa miongoni mwa wazungumzaji katika mikutano tisa ya waandishi wa habari iliyofanyika Soccer City na viwanja vingine.
Mechi za Kombe la Dunia zimefanyika kwa siku 24, na kila mwandishi alitakiwa kuona mechi moja kwa siku, niliona mechi 22, ingawa nilitakiwa kuona mechi 24, lakini sikwenda kuona mechi mbili kwa sababu maalumu. Mechi ya kwanza ambayo niliingia mitini ni nusu fainali ya kwanza kati ya Uruguay na Uholanzi kwenye Uwanja wa Green Point mjini Cape Town umbali wa ni saa 14 kwa basi kutoka Johannesburg.
Sikwenda katika mechi hiyo iliyokuwa inachezwa usiku wa Jumanne kwa sababu usiku huo nilikuwa safarini kutoka Johannesburg kwenda Durban kushuhudia mechi ya nusu fainali ya pili kati ya Hispania na Ujerumani kwenye Uwanja wa Moses Mabhida iliyokuwa inafanyika Jumatano usiku. Tuliondoka Johannesburg saa tatu usiku Jumanne na kufika Durban saa 12:00 asubuhi Jumatano.
Baada ya mechi kati ya Ujerumani na Hispania, kwisha saa 4:30 usiku, tulikwenda moja kwa moja katika kituo cha mabasi na kupanda basi la kurejea Johannesburg ambako tulifika saa moja asubuhi Alhamisi.
Tukiwa tumetumia siku mbili kulala kwenye basi. Ratiba kama hiyo ilijirudia mara kwa mara kwa karibu siku zote za mashindano.
Sikwenda mjini Port Elizabeth ambako ni mwendo wa saa 15 kwa basi kwenda kutazama mechi ya mshindi wa tatu kati ya Uruguay na Ujerumani, badala yake nilibaki Johannesburg kufanya kazi za ofisi huku nikiisuburi fainali kati ya Uholanzi na Hispania.
Namshukuru sana Tenga kwa kunipa moyo wakati nilipokutana naye mara tatu katika mechi ya Paraguay dhidi ya Japan, nusu fainali kati ya Hispania na Ujerumani na kwenye mkutano wa waandishi wa habari Soccer City.
Haikuwa kazi rahisi lakini kwa sababu ya kuwa na waandishi wengine marafiki zangu kama Fred Kaweesi wa gazeti la New Vision la Uganda na Mukoka wa gazeti la The Post la Zambia, tulijikuta tukifanya kazi nzuri na kwa ushirikiano mkubwa jambo ambalo lilifanya kazi iwe rahisi.
Baada ya mechi ya fainali baina ya Hispania na Uholanzi, nilifurahia kuhudhuria mkutano wa waandishi wa habari ambao uliitishwa na Rais wa Fifa, Sepp Blatter siku inayofuata yaani Jumatatu. Alizungumza mengi.
Ingawa wengi wanaweza kudhani nimefaidi kuona Kombe la Dunia, lakini kwangu ilikuwa ni kazi ngumu na iliyonipa changamoto kubwa katika fani ya uandishi wa habari.
mwisho