MICHAEL MOMBURI
ORLANDO Pirates ya Afrika Kusini imo katika programu ya kuinoa Yanga ambayo inajiandaa kwa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kocha wa Yanga, Kosta Papic amesisitiza kuwa anahitaji mechi sita kabla ya kuanza kwa ligi na moja ya programu yake itakuwa ni kucheza na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
"Tutacheza kwao ugenini au hapa Tanzania, lakini ninataka mechi sita za kirafiki; nne za kimataifa na mbili za ndani," alisema Mserbia huyo.
"Tunaweza kwenda Afrika Kusini, Uganda na Kenya au wao wakaja kwetu," alisema Papic ambaye ni kocha wa zamani wa Orlando Pirates na Kaizer Chiefs.
Papic ametamba kuwa anataka kucheza na Simba wakati wowote hata iwe sasa na kwamba mechi yao ya Ngao ya Hisani imekuja wakati muafaka.
Bosi huyo ambaye timu yake ilionyesha uwezo mkubwa wa kupiga pasi nyingi mazoezini jana Ijumaa asubuhi, aliweka wazi kuwa amesajili kikosi imara na muafaka kwa fomesheni yake ya 4-4-2 ambayo ni kushambulia zaidi.
Yanga iliyopangwa kucheza na Simba, Agosti 14 katika mechi ya Ngao ya Hisani, inajifua kwenye Uwanja wa Uhuru huku Papic akisema kuwa mabadiliko ni makubwa na anazidi kuumiza kichwa kuimarisha mambo ya ufundi.
"Vijana wapo tayari kucheza na Simba wakati wowote, naipa hiyo mechi umuhimu wa kawaida, naichukulia kama mechi ya kirafiki dhidi ya timu yoyote ya Tanzania hii," alisema Papic huku akimsifu kipa Mserbia kwa madai kuwa ameonyesha kiwango cha juu.
Katika hatua nyingine, kiraka huru wa SC Villa ya Uganda, Hood Mayanja ndiye mchezaji gumzo kuliko wote wapya waliosajiliwa na Yanga kutoka nje kutokana na mambo yake adimu mazoezini kila kukicha yaliyowafunika hata Waghana Kenneth Asamoah, Ernest Boakye na Issack Boakye.
Hood hajasajiliwa kucheza Ligi Kuu, lakini Papic ameahidi kumuhifadhi pamoja na Mkenya Anene hadi dirisha dogo ingawa mashabiki walitaka aondolewe Issack ili Mayanga apewe namba kwa vile anapiga pasi za uhakika na anacheza anavyotaka ingawa kitendo cha kusifiwa mno kilifanya baadhi ya wachezaji kumfanyia vimbwanga.
Mayanja ambaye anasifika zaidi akicheza beki ya kushoto aliiambia Mwanaspoti kuwa; "Nitabaki Yanga mpaka dirisha dogo, lakini itategemea kama watakuwa tayari kunilipa mshahara, nitakuwa na kikao nao leo (jana Ijumaa) jioni."
mwisho