MSANII Kidumu wa Burundi anayetamba na wimbo wa 'Haturudi Nyuma' amewashauri wasanii wa filamu nchini kufikiria kuliteka soko jijini Kigali, Rwanda na Bujumbura, Burundi kutokana na mapenzi yaliyoonyeshwa na raia wa huko.
Kidumu aliwaambia wasanii aliokutana nao kwenye Tamasha la Nchi za Majahazi, ZIFF mjini Zanzibar akisema kuwa yeye ni mmoja katika ya maelfu ya mashabiki wa filamu za kibongo.
Msanii huyo alisema Tanzania ina nafasi kubwa ya kuliteka soko la Rwanda na Burundi kwa kuwa nchi hiyo inazungumza Kiswahili na Kifaransa na filamu nyingine zote zinatumia kiingereza.
“Rwanda wanapenda filamu za Kiswahili sana kwa kuwa ndiyo lugha wanayoielewa, filamu za Nigeria na Marekani hawazitazami kwa kuwa hawaifahamu lugha ya Kiingereza, nawashauri muangalie namna ya kuliteka soko la filamu la kule,” alisema Kidumu.
Aidha aliwashauri wajaribu kuwashirikisha wasanii kutoka kule pamoja na kutunga hadithi za maisha ya watu wake na si kusubiri watu watoke Ulaya watengeneze filamu kama vile Hotel Rwanda.