Na Julieth Kulangwa, Zanzibar
BAADA ya kupata Tuzo ya Mwigizaji Bora Tanzania ya ZIFF, msanii wa maigizo wa siku nyingi, Yvony Cherry maarufu kama Monalisa amewacharukia wanaowasema vibaya kwa kuwataka wawaache kama walivyo kwani wanajua wanachokifanya.
Monalisa amesema Watanzania wamekuwa wakiangalia filamu kwa jicho la kukosoa badala ya kuangalia kitu kizuri ambacho wanakifanya, na ndio maana wanabaki kusema badala ya kujifunza.
"Tunajitahidi kufanya kazi nzuri kuwaridhisha Watanzania, lakini wenzetu wamekuwa wakosoaji wakubwa, hakuna zuri wanaloliona kwenye kazi zetu ingawa wanajua ugumu tunaokutana nao kila siku.
"Wanahoji kwanini tunaigiza kwenye majumba makubwa na magari ya kifahari, kwani haya majumba na magari sisi tunayatoa wapi, si hapa hapa Bongo sasa kwanini wahoji kwamba tunaiga kutoka Nigeria?" Alihoji Monalisa.
Monalisa amewaomba mashabiki wa filamu kutoa mchango kwa kununua nakala halisi ili sanaa hiyo iendelee kukua kwani wizi wa kazi zao ndio sababu kubwa inayosababisha soko lao kuwa dogo.
"Tunawaomba Watanzania wanunue nakala halali ili tuendelee kufanya kazi nzuri, kama wakinunua nakala halali nasi kipato chetu kinaongezeka kwa maana hiyo filamu zijazo zitakuwa nzuri tofauti na sasa.
"Ni takribani miaka kumi sasa tangu soko la filamu lianze nchini, lakini bado tunatengeneza filamu kwa bajeti zilezile kwa kuwa soko halikui na wezi wanaongezeka, tunawaomba Watanzania watusaidie kwa hili halafu mengine tutafanya sisi," anasema Monalisa.
Monalisa, ambaye ni mmoja kati ya waasisi wa maigizo ya kwenye runinga na filamu amesema kwa zaidi ya miaka kumi aliyokuwemo kwenye fani ya uigizaji, ameishi kama muigizaji na si msanii kama walivyowaigizaji wengine na ndio maana jina lake limekuwa kwenye chati kwa kipindi chote hicho.
Muigizaji huyo, ambaye sasa ameigiza filamu ya'Binti Nusa' akiwa muhusika mkuu amesema, tunzo hiyo inamaanisha kuwa yeye ni bora kuliko waigizaji wote nchini kwa wakati huu.
"Ninastahili kupata tuzo hii na nyingine kwani ni mmoja kati ya waigizaji mahiri nchini, filamu zote zimepata nafasi ya kuigiza kwa sababu ninaiweza kazi hii na si kama wengine ambao wanapewa nafasi kwa sababu fulani."
Monalisa anasema tuzo hiyo imetolewa kwa muigizaji bora Tanzania na yeye ameonekana kuwa bora kutokana na kazi zake nzuri zinazotambulika.
"Usanii una maana nyingi, hasa hapa kwetu Bongo ambako neno hili linatumiwa likimaanisha kuwa matapeli, ndio maana nakataa kuitwa msanii ingawa kwenye tasnia hii kuna watu wanastahili kuitwa wasanii,
"Kama mtu ameingia kwenye fani hii kwasababu anatafuta jina kwanini asiitwe msanii? Kama msanii ameingia kwenye fani hii kwa sababu amekosa kitu kingine cha kufanya kwa nini asiitwe hivyo?" Anahoji Monalisa.
Muigizaji huyo aliyejipatia umaarufu akiwa na Kundi la Mambo Hayo amesema fani ya uigizaji inalipa kama ikitumiwa vizuri na kila mmoja atasimamia haki yake ipasavyo, alisema kuna wasanii wapo tayari kufanya kazi hiyo bure ili mradi tu waonekane kwenye runinga.
"Wauza sura ndio wanatuharibia kazi wakati mwingine, unakuta msichana mzuri anakubali kuchezeshwa bure ilimradi tu aonekane kaigiza na mtu fulani, lakini kama wote tutakuwa na msimamo mmoja kazi itakwenda vizuri.
"Vilevile watayarishaji wa filamu nao kama hawatakuwa na njaa ya pesa ndogo ndogo wanaweza kutengeneza filamu nzuri zaidi ya hizi za sasa," anasema Monalisa.