KIUNGO wa Ghana, Laryea Kingston amemuomba radhi Naibu Waziri wa Michezo, Nii Nortey Dua kutokana na kauli zilizotolewa na mama yake (Laryea).
Mama yake anadaiwa kumrushia matusi naibu waziri huyo baada ya Kingston kutemwa kwenye kikosi cha wachezaji 23 walioenda Afrika Kusini kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Akizungumza na tovuti ya Joy Sports, Waziri huyo alisema kuwa alipigiwa simu na Kingston wakati timu ikiwa kambini Scotland na akaomba radhi.
Nii Nortey Dua, ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Ledzorkuku alielezea kuwa tukio hilo ni la kawaida katika kazi yake.
"Nilishasahau suala hilo hata kabla ya kupigiwa simu," alisema.
Kingston alikulia kwenye jimbo hilo hadi alipoanza kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.