JOHANNESBURG, Afrika Kusini
IMEKUWA ni wiki ambayo soka la Tanzania limeingia kwenye ramani ya dunia baada ya ujio wa Brazil, Jumatatu iliyopita lakini haijaishia hapo Watanzania wanapaswa kufurahia zaidi kutokana na kuwa na mwakilishi kwenye Fainali za Kombe la Dunia.
Watanzania baada ya kutangazwa kuwa fainali hizi zitafanyika nchini Afrika Kusini walitaka kuona moja ya timu zilizofuzu angalau kwa sababu Taifa Stars ilitolewa mapema.
Beki wa kushoto, Patrick Mtiliga, ambaye ni jina miongoni mwa Watanzania atapeperusha bendera ya Tanzania kwenye fainali hizo.
Mtiliga, ambaye baba yake ni Mtanzania atavalia jezi ya Denmark, kwa sababu ndio asili ya mama yake.
Mtanzania huyo, ambaye atashangaza wengi kutokana na mashabiki wa soka kutofahamu habari zake, anachezea Malaga ya Hispania, ambayo inashiriki La Liga.
Mtiliga, alipatwa na mkasa baada ya kuvunjwa pua na nyota wa Real Madrid, Ronaldo kwenye mechi ya La Liga.
Katika mchezo, ambao Ronaldo alizamisha mabao yote mawili, alijikuta akitolewa kwa kuonyeshwa kadi nyekundu na kusimamishwa mechi mbili.
Kwa mujibu wa mtandao wa Shirikisho la soka la Kimataifa (FIFA), atatumiwa kwa nafasi ya beki wa kushoto na Kocha wa Denmark, Morten Olsen.
Olsen inadaiwa katika siku za karibuni amekuwa akihangaika kuziba nafasi ya beki wa kushoto na kujaribu wachezaji kadhaa kama Chris Sorensen, Michael Lumb na Leon Jessen.
Kwa mshangao wa wengi amemjumuisha Mtiliga, ambaye amechezea timu hiyo mara tatu tu.
Hata hivyo, kujumuishwa kwa Mtiliga kwenda Sauzi kwa kiasi kikubwa ni kitendo chake kuchezea mara 27 timu za vijana za Denmark kiasi cha kuitwa kwenye timu ya taifa kwa mara ya kwanza Novemba 2008 wakati timu hiyo ilipocheza na Wales.
Mtiliga aliyezaliwa Januari 28, 1981, alijiunga na Malaga kutokana na kujituma wake na amewahi kuzichezea timu maarufu kama FC Copehnagen, Feyenoord na NAC Breda za Uholanzi.
Kuna Watanzania wengi tu wamekwenda nje kucheza soka na kuchukua uraia lakini hawakufikia mafanikio ya kucheza Kombe la Dunia.
Ni pamoja na Nicodemus Njohole na Kassim Manara (Austria), Hilal Hemed, Ahmed Amasha, Yussuf Abeid, Twalib Hilal na Thuwein Ally (Oman).
Mtiliga alizaliwa Copenhagen na alianzia soka yake akiwa na yosso katika klabu ya Boldklubben 1893.
Alianza soka akiwa kama mshambuliaji na mara nyingine alipangwa na makocha kama kiungo mshambuliaji.
Alipata nafasi ya kucheza soka ya wakubwa katika msimu wa 1998-99.
Baada ya mechi 13, alihamia Feyenoord Rotterdam ya Uholanzi na kucheza Ligi Kuu ya nchi hiyo.
Baadae Feyenoord iliamua kumtoa kwa mkopo katika klabu yao ndogo ya Excelsior Rotterdam na kucheza katika ligi za madaraja ya chini.
Alichezea timu hiyo kwa misimu minne na kusaidia kupanda Ligi Kuu Uholanzi katika msimu wa 2001-02 ingawa baadae ilishuka daraja. Katika msimu wa 2003-04, alikuwa akipangwa katika kikosi cha kwanza na kuitwa tena katika Feyenoord.
Alicheza mechi 11 kwenye Ligi Kuu Uholanzi lakini msimu huo alipata pigo baada ya kuumia paja mwaka Januari 2005.
Alipona Januari 2006, Feyenoord ilitaka kumtoa tena kwa mkopo lakini Mtiliga aligoma na kubakia kwenye kikosi cha pili.
Mwezi Agosti 2006, Mtiliga alihamia NAC Breda kwa mkataba wa mwaka mmoja lakini baada ya kung'ara na timu hiyo aliongezewa mkataba.
Katika msimu wa 2007-08, alicheza mechi 30 kati ya 34 wakati NAC iliposhangaza wengi na kukamata nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu Uholanzi.
Aling'ara na kutokea kati ya mabeki bora wa kushoto kwenye ligi na mkataba wake ulipomalizika mwaka 2009 klabu nyingi zilitaka kumsajili.
Alisaini mkataba wa kujiunga na Malaga CF ya Hispania ili kucheza kwenye La Liga katika msimu wa 2009.
Aliumia kwenye mchezo wake wa kwanza na alikuwa na wakati mgumu kurejea kwenye kikosi cha kwanza.
Alitakiwa kuhakikisha anasaidia mashambulizi ya timu yake na kocha Juan Ramon Lopez Muniz na baadae alipata nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Alipata mkataba Januari 24, 2010 kwenye mechi ya La Liga dhidi ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo alimvunja pua baada ya kumpiga kwa kiwiko kwenye uso.
Ronaldo alitolewa kwa kuonyeshwa kadi nyekundu na Mtiliga alilazimika kukaa nje ya uwanja kwa wiki tatu.
Mtiliga alianza kutambulika kwenye soka la kimataifa Agosti 1997.
Alichezea timu za yosso mara 28 na kufunga mabao manne kwa timu ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 na bao moja kwa timu ya wenye umri wa miaka 21.
Katika kipindi chake alichokuwa Feyenoord, Mtiliga alikuwa anatakiwa na timu ya taifa ya Uholanzi.
Aliitwa kwa mara ya kwanza kwenye timu ya taifa ya wakubwa wa Denmark, Novemba 2008, alipoitwa na kocha Olsen.
Mechi yake ya kwanza ya timu ya taifa ilikuwa dhidi ya Wales, lakini baadae aliachwa kwenye kikosi hicho.
Aliitwa kwenye kikosi cha Denmark kwa mara nyingine Mei 2010, kwa ajili ya kikosi cha kushiriki kwenye Fainali za Kombe la Dunia.
Kuteuliwa kwake kulishangaza wengine ingawa aliitwa kutokana na Olsen kugundua alikuwa na kiwango bora baada ya kung'ara na Malaga.
Mambo yalizidi kumnyookea zaidi baada ya kutajwa katika kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 cha Denmark kitakachoshiriki kwenye Fainali za Kombe la Dunia.
Factbox
Jina: Patrick Jan Mtiliga
Kuzaliwa: Januari 28, 1981
Mahali: Copenhagen, Denmark
Urefu: 1.71 m
Nafasi: Beki wa kushoto
Klabu: Malaga
Namba: 19
Taifa: Denmark