MUSSA MKAMA
MUZIKI wa mwambao kwa sasa umeshika kasi nchini. Muziki huo umekuwa ukijizolea sifa kila kukicha kwa vile umejaa maneno mengi ya mipasho, ambayo mara nyingi hupendwa na watu wa uswahilini.
Lakini kuna dhana iliyojengeka kwamba wanamuziki wa mipasho wanatoa maneno hayo kwa kuwa maisha yao halisi yamezungukwa na mambo ya aina hiyo.
Hata hivyo muimbaji wa Kundi la Five Star Modern Taarab, Zuwena Mohamed anakanusha dhana hiyo kwa kuanika kuwa kusengenya au kutoa maneno ya mipasho mitaani ni hulka ya mtu.
"Mimi ni miongoni mwa watu wasiopenda fitina na majungu ninaweza kuimba maneno mipasho lakini maisha yangu halisi si hayo.
Anasema ni kweli kuna baadhi ya waimbaji wamejaa majungu na fitina lakini si wote.
“Naogopa sana kuitwa mmbea, sipendi kuwa hivyo, ninaepukana na makundi yasiyo na sababu kwa kuwa ndiyo chanzo cha yote,” anasema Zuwena.
Mwimbaji huyo wa mipasho anasema katika maisha yake hatarajii kuingia katika magenge ya umbea na kufitini watu, kwa sababu kitendo hicho kinasababisha mtu kuwa mchawi.
“Ukiwa na makundi ya kufitini lazima utakuwa na wivu. Wivu ukizidi utaaanza kujiingiza kwa waganga wa kienyeji na kutumia nguvu za giza na hapo ndipo utakapobobea katika uchawi,” anasema Zuwena.
“Taarab lengo lake ni kutoa burudani na mafunzo, kama katika wimbo kukiwa na maneno ya mitaani, basi lengo ni kuongeza ladha lakini si kukuza umbea,” anasema Zuwena.
“Unajua hakuna adui mkubwa duniani kama fitina, umbea na makundi yasiyo na sababu, ukiona hali hiyo inajitokeza jiepushe mapema kwani ni hatari kama bomu la nyukilia,” anasema Zuwena.
Mwimbaji huyo, ambaye kipaji chake kiligundulika kwenye harusi wakati Kundi la Super Shine likitumbuiza huko Zanzibar mwaka 1999, amesema binadamu hapaswi kuwa na tabia kama hizo kwani hayo ni mambo ya shetani.
“Nahitaji kuwa muimbaji mkubwa kama Bi Kidude na ili kufikia huko natakiwa kuachana na mambo ya ajabu mapema," anasema Zuwena.
Na mwanamuziki huyo anasema kuwa hivi sasa muziki huo unaboreshwa zaidi na baada ya muda mfupi watu wataelewa kwamba taarab si kisima cha umbea.
Akielezea safari yake katika muziki huo, Zuwena anasema aliibuliwa katika fani na kikundi cha Super Shine.
"Kuna siku walikuwa wakitumbuiza, kiongozi wa kundi hilo aliomba kama kuna mtu aliyefahamu kuimba nyimbo zao, nami sikuona hiyana nilikwenda jukwaani na kushusha mistari.
"Baada ya hapo walinichukua kwa ajili ya majaribio, nilizunguka nao katika matamasha mbalimbali na kupata uzoefu.
"Baada ya kutamba, kiongozi wa Kundi la Jahazi Modern Taarab, Mzee Yusuf alininyanyua nikaimba kwa muda kabla ya kuhama tena," anasema dada huyo ambaye kabla ya kujikita katika taarib alikuwa akifanya kazi ya kuwachora maharusi kwa hina na kuwapamba.