Na Dismas Lyasa
NDOA ni muungano wa mwanamke na mwanaume ambao wameamua kuishi pamoja kisheria.
Na msingi wa kuwa na maisha bora, ni kuheshimiana na kila mmoja ajione anayo haki ya kumpenda mwenzi wake.
Kwa wakati huu familia zinakabiliana na changamoto mbali mbali zinazochangia kuharibika kwa ndoa nyingi zikiwemo baadhi yao kuiga mambo ya kigeni, lakini ni wajibu wa wanandoa kusimama kidete kutetea, kulinda na kuimarisha ndoa zao.
Msingi wa kuwa na maisha ya amani ya ndoa ni kwa kila mwanandoa kujiona kuwa analo deni kubwa la kuilinda na kuiheshimu ndoa yake. Je, unayofanya yanalinda ndoa yako? Jiulize mwenyewe kisha chukua hatua.
Ninachotaka kusema hapa ni kuwa katika ndoa unapaswa kutegemea furaha, lakini pia ni vizuri kujiuliza je, vipi kama itatokea taabu? Je, utachukua uamuzi gani?
Jambo jingine la kutafakari sana ni juu ya kauli na matendo yako. Wakati fulani watu huharibu ndoa kwa kauli zao wenyewe. Kwa mfano kuna mwanaume kwa miaka mingi amekuwa mwenye matendo mabaya ya kwenda nje ya ndoa, baadaye akaamua kuachana na tabia hiyo.
Hakuishia hapo, hakuwa anakwenda hata kwenye nyumba ya ibada, akaanza kwenda na mkewe, ambaye alikuwa akienda sana kuomba Mungu ili mumewe aipende ndoa yao.
Siku moja wakiwa na amani, mke akaanza kuiharibu ndoa kwa maneno yake. Unajua ni maneno gani? Ni maneno machache sana…kwamba “aaah bila mimi kuwa imara katika maombi usingebadilika na kuendelea kuiheshimu ndoa yetu’.
Kwa haraka unaweza kuona kama ni neno lisilo na nguvu, lakini ukweli ni kwamba tangu siku hiyo lilianza kuiharibu ndoa hiyo…mume aliuliza “aaah kwa hiyo wewe ndio umechangia nimekuwa na mabadiliko yote haya katika maisha, yakiwemo maendeleo”….Mke alijibu “eeeh nimekuwa nikikuombea sana”.
Je, ndugu yangu umejifunza nini hapa? Ni kwamba ulimi umechangia kuharibu uhusiano. Ukweli ni kwamba katika kusahihishana unapaswa kuwa makini sana. Kwa asili yake, wanaume walio wengi huwa hawapendi kuonekana kwamba wamerekebishwa jambo fulani baya na wanawake.
Huwa hawapendi kuonekana kwamba wako juu ya wanawake kwa namna yoyote ile. Kama unafanikiwa kumbadilisha mumeo, huna sababu ya kujigamba mbele yake, tahadhari sana, jua kwamba kitendo chako hicho kitachangia kuharibu, wala sio kujenga. Hiyo pia iko kwa wanawake.
Kimsingi si vizuri kujifanya wewe ni bora zaidi ya mwingine. Uwe makini sana na ulimi wako, hata kama anaanza kukusifia, mwambie aaah hapana mpenzi wangu, ni jitihada zako hizi. Acha mwenzi wako akusifie kwa mazuri unayomtendea, sio kujisifia mwenyewe.
Ninachotaka kusisitiza ni kwamba ndoa ili uifurahie ni lazima uwe makini sana. Ndio huwa nasisitiza kwamba wakati fulani unapaswa kukaa na washauri kuzungumza nao namna unavyopaswa kuendesha ndoa yako hata kama kuna amani ya kutosha, ili wakusaidie kuifanya iendelee kuwa na amani zaidi.
Kama kweli unataka kuwa na ndoa yenye amani, ni lazima uchukue hatua za kuhakikisha unakuwa na ndoa yenye amani. Pia fahamu ya kuwa ni kweli tunaingia kwenye ndoa ili kupata raha, lakini raha huwa haiji yenyewe kama upepo, ni lazima uendelee kufanya jitihada za kuipata hiyo raha.
Kama unafikiri ndoa ni raha tu, ndoa ni amani tu, nakushauri usiingie kwenye ndoa. Kama nilivyosema kuwa ni kweli tunaingia katika ndoa kwa lengo la kuwa na amani, lakini pia elewa kuwa migogoro ni vitu ambavyo hutokea katika maisha.
Nina maanisha kuwa elewa namna ya kusuruhishana katika migogoro. Kukwaruzana si mwisho wa ndoa. Maana kuna wanandoa wakikwaruzana kidogo, wanaanza kutoleana matusi ya nguoni nk, wanashindwa kuelewa kwamba wakati mwingine migogoro ni vitu vya kawaida, kitu cha msingi ni kusameheana na kuendelea na uhusiano.
Wanandoa wanatakiwa kujua mbinu za kufanya ili wasichokane. Sababu kubwa ya wanandoa kuchokana, ni pale mmoja au wanandoa wote wanaposhindwa kutumia nafasi zao kuleta utulivu katika ndoa yao.
Aidha ndoa yoyote ambayo watu wake hawaheshimiani au hawaishi kwa kuzingatia misingi ya dhati ya dini, husababisha wanandoa kuchukiana. katika zama tulizonazo zama ambazo umagharibi umetawala katika mila na desturi zetu, watu wengi ukiwauliza watakuambia ni wa dini fulani, lakini wanapuuza mafundisho yao; Dini inaonekana ni imani ya kuzaliwa nayo, na si matendo na utaratibu wa maisha ya mtu.
Kuna watu wanatafsiri vibaya mafundisho ya Mungu, kwa mfano kuna watu wanaamini kuwa Muislamu, ni kuvaa hijaab, hata kama haswali, fedhuli…eti ili mradi amezaliwa Muislamu basi huyo ana dini, ufahamu huu umewaingiza wanandoa wengi katika mitihani.
Hata katika Ukristo kuna watu wanaitwa Wakristo kwa sababu tu wamezaliwa familia za Kikristo. Ndio kusema kuna watu wanavaa Hijaab kama sehemu ya mila, na anaswali swala tano kutokana na makuzi yake. Kuna mabinti au wanaume wanakwenda kanisani au misikitini kwa sababu ya kushinikizwa na wazazi au walezi wao, lakini wao wenyewe hawana hofu na Mungu hata kidogo.
Hivyo basi, ni muhimu kwa wanaotaka kuoana wahakikishe kama kweli wanataka kuchagua kwa misingi ya dini zao, kuwa makini kwa kuhakikisha kweli wanapata aina za watu wanaowataka hasa kwa kuangalia mavazi na matendo yao. Jipe muda wa kuchunguzana, wala haraka haina baraka, kama anaharaka ruhusu aendelee na safari, kama ni bahati yako utaipata, si ndio jamani?
Dismas Lyassa ni mtaalam wa uhusiano, wasiliana naye 0754 498972.