KILA mwenye kuamini kuwa yuko kwenye ndoa ajiulize je, yuko kwenye ndoa halali? Jipatie majibu mwenyewe.
Kama unafikiri uko kwenye ndoa halali jiulize ni kwa nini unaamini hivyo na kama pia unaamini hauko kwenye ndoa halali pata jibu ni kwa nini hauko kwenye ndoa halali.
Lakini lililo la msingi zaidi ni kujua nini la kufanya ili uwe na ndoa halali.
Kuna wanaume katika maeneo mbalimbali nchini wanaishi na wanawake hata hawajawatolea mahari wala hawajajitambulisha kwa wazazi wa hao wanawake wanaoishi nao, nao wanataka wajulikane kuwa nao wameoa.
Mimi sipingi hili, maana sheria ya ndoa inasema ukikaa na mwanamke kwa zaidi ya miezi minane nafikiri, watu wakiamini kuwa ninyi ni mke na mume, basi tayari ni wanandoa. Je, ni kweli katika maisha ya kawaida unatakiwa kuwa na aina hii ya ndoa?
lengo la makala haya leo ni kwa kila mwenye ndoa kutafakari, nawe pata muda wa kutafakari juu ya kama uko kwenye ndoa halali au la. Kama ni yule ambaye anaishi tu na mwanamke bila kujitambulisha kwao, endelea kutafakari ndugu yangu na mwombe Mungu akupe hekima, jiulize vipi siku kijana atakapokuja kumchukua binti yako bila kufuata utaratibu wowote, utafurahi? Je, ni halali pia kwamba watu wamenalihiana weeeee….hadi wanaanza kukinaina ndio wanakwenda kanisani au msikitini kuoana? Ni mambo ambayo wewe unayesoma makala haya unatakiwa kupatia majibu.
Ni wazi wewe umekuwa ni shahidi wa baadhi ya ndoa za watu kwamba wamekuwa wakiishi pamoja kwa miaka mingi, au wengine wameshatiana uja uzito. Je, ni kweli tunapaswa kuwa na aina hizi za ndoa?
Wengine wanaita kubarikiwa kwa ndoa, kwamba wameishi hivi hivi kwa miaka mingi, kisha wameshazaa watoto kibao au labda hawana, bali wameishi miaka mingi pamoja kama mke na mume. Kitaalam ni sahihi kuwa hivi? Mbaya zaidi ni kwamba wengi wenye kufanya hivi ni wale ambao wako kwenye dini iwe ya ukristo au uislam.
Jibu la swali hili ni kwamba kwa misingi ya dini zote, lililo la msingi ni kwamba kama mwanamke na mwanaume wamependana, kuna taratibu za kufuatwa, kwa mfano kwa mwanaume kwenda kujitambulisha kwa wazazi wa mwanamke, kisha kutoa mahari na baadaye kwenda kuonana na kiongozi wa dini wanayoiamini ili abariki huo uamuzi wao wawe mke na mume rasmi.
Kuishi na mwanamke bila kujitambulisha kwake au kukataa kumtolea mahari, ni uhuni, ni kudharauliana na kwa ujumla ni kuhatarisha mwenyewe uhusiano wako.
Mbaya zaidi kuna wanaume wana ulimi mchafu, utakuta anamwambia mwanamke aaa acha kunibabaisha, sina mpango wa kutoa mahari wala kujitambulisha kwenu, kama unataka kuondoka nenda. Kuna wengine wanakwenda mbali zaidi wakitoa majigambo “Wewe ukiondoa leo, kesho naleta mwanamke mwingine, akuoe nani wewe umeshazeeka, umeshazaaa”.
Kuna wanaume wamekuwa na kauli za kipuuzi kama hizi. Mwanaume huyu-huyu anayetoa kauli chafu, siku mbili baadaye anagombana na dada yake kisa ana uhusiano na mwanaume, lakini haji nyumbani kujitambulisha.
Mkuki kwa nguruwe, kwa binadamu uchungu. Ndugu zangu wanaume, jambo la msingi sana unapokuwa na mwanamke na kama umeridhika naye kweli, si hadi mwanamke aanze kukwambia, bali unapaswa kuacha mchakato wa kuoana uanze ambao kwanza ni kumuandaa mtu ‘mshenga’ wa kwenda kujitambulisha kwa wazazi, kutoa mahari na pia kwenda kwa mchungaji.
Mnaweza kufunga ndoa, sherehe ni maamuzi ya watu wenyewe, mnaweza kuifanya hata kama ni kwenye kutumiza mwaka au hata zaidi. Ni suala la kuamua, mnaweza kuwaita watu wachache muhimu na kuwaeleza haya na kufurahia maisha. Ufahari katika kuendesha harusi si jambo la msingi sana, lililo la msingi ni kutumiza matakwa ya dini unayosema unaiamini.
Je, makosa makubwa, mtu anasema ni wa dini fulani, halafu anaishi na mwanamke au mwanaume pasipo kufunga ndoa, sababu eti hana fedha. Ndugu zangu ndoa ni suala la kumuona kiongozi wa dini yako, kuzungumza naye, kisha anawapangia siku ya kwenda kufunga, sio lazima mfanye sherehe.
Ingawa ni kweli tukio hili la kuoana ni la msingi kwa hiyo linapaswa kuendeshwa kwa staili ya peke yake, usilazimishe mambo, usimuige tembo, eeeh ndugu yangu, fanya mambo kulingana na uwezo.
Vipi kuhusu kuwahusisha wazazi katika mpango wako wa kutaka kuolewa au kuoa? Kitaalam ni vizuri kuwashirikisha wazazi na ni jambo la furaha zaidi pale wanapokubaliana na mtu ambaye unataka kuoana naye.
Hata hivyo, kama hawataki bado unaweza kuoa au kuolewa lakini jitahidi kuwaelewesha msimamo wako na uendelee kuwapenda na kuwasisitizia kwanini unaona ni muhimu kuchukua uamuzi huo wa kuoa au kuolewa na mtu huyo.
Jambo la kuzingatia ni kwamba mara nyingi uwe makini na ushauri wa wazazi, wengi wanashauri kwa kukutakia mema,hana sababu za kukataa, tafakari kwa makini wanapokataa, ingawa wengine huwa hawana sababu za msingi, hata vitabu vitakatifu vinasema “Enyi watoto watii wazazi wenu, mpate miaka mingi na maisha ya heri".
Ninachotaka kusisitiza hapa ni kwamba ndoa halali ni ile inayopata baraka za wazazi ( japo si lazima, ingawa ni muhimu sana). Hata hivyo, ni muhimu katika maisha kuwa makini na kila anayekushauri, kwa sababu ni ukweli kwamba kuna mzazi haina maana kwamba tayari una elimu au shahada ya ushauri, kuna wazazi wengi wanahitaji kushauriwa.
Wakati mwingine wazazi wanataka kutimiza mambo ya mila, huenda wakati huo mtoto amejiimarisha katika dini, tumia hekima, si vizuri kumkwaza mzazi, kama si lazima kufanya hivyo. Je, ukifungiswa ndoa bomani ni halali hiyo ndoa kwa misingi ya dini? Kwamba aaah bwana eeeh wewe wa dini fulani na mimi fulani, kwa hiyo kila mtu akae na yake.
Ukweli ni kwamba kuangalia mmefungia wapi ndoa sio muhimu sana, ingawa ni muhimu, lakini la kuzingatia zaidi ni hali halisi ya maisha baada ya wanandoa kuanza kuishi pamoja. Wanandoa wanapaswa kuelewana na kuzifukia kasoro zao, kuwa na muda wa kuzungumza kuhusu ndoa yao na namna gani wanaweza kwenda mbele bila mmoja kuwa na kinyongo.
Dismas Lyassa ni mtaalam wa uhusiano aliyesajiliwa na serikali (Social Welfare Counselor), 0712183282 Mwisho