KOCHA wa Yanga, Kostadin 'Kosta' Papic amemwambia Athuman Idd 'Chuji': "Usikubali kwenda Lupopo, wewe ni mchezaji wa Ulaya." Lakini Chuji amemwambia kocha huyo: "Hapana, hapana, mie naangalia maisha bwana."
Kocha huyo wa zamani wa Orlando Pirates ya Afrika Kusini amepigilia msumari wa mwisho na kusema kuwa kama Lupopo waking'ang'ania watatakiwa kutoa Shilingi 180 kumpata kiungo huyo.
Alisema Lupopo watatakiwa kutoa dola 100,000 (Sh milioni 120) kwa Yanga na dola 50,000 (Sh milioni 60) kwa Chuji.
"Kama Lupopo waking'ang'ania watatakiwa kutoka dola 100,000 kwa Yanga, dola 50,000 kwa Chuji na mshahara wa dola 5,000 kila mwezi kwa Chuji," alisema Papic ambaye katika tangazo la televisheni ya Supersport huonekana akicharuka, lakini ni enzi alipokuwa Hearts of Oak ya Ghana.
Chuji alipozungumza na Mwanaspoti jana Jumatatu mchana alikiri kuzungumza kwa kina na viongozi wa juu wa Lupopo akiwemo rais wao, lakini hakuweka bayana alichoahidiwa.
"Nimezungumza nao sana, na mimi ninawasikiliza watakujaje kama mambo yakienda sawa , niko tayari dakika yoyote, natafuta masilahi si vinginevyo," alisema mchezaji huyo na kuongeza kuwa viongozi hao wamemwambia wanakuja Dar es Salaam muda wowote.
"Huu ndio wakati wangu wa kufanya kazi na kujenga maisha yangu na mpira sasa umekuwa masilahi zaidi."
Akizungumza na Mwanaspoti, Papic ambaye Afrika Kusini, Nigeria na Ghana anaitwa Clinton alisema kiwango cha Chuji si cha kufikiria kucheza soka katika nchi za Afrika.
"Anatakiwa kwenda kucheza soka Ulaya, aache kufikiria kucheza Afrika," alisema Papic ambaye wikiendi iliyopita timu yake iliifunga Azam FC mabao 2-1.
"Wachezaji wengi wa Simba na Yanga, hadhi yao ni ya kucheza Ulaya, wanatakiwa kubadilika kimtazamo tu, wabadike kitabia ndani na nje ya uwanja, vinginevyo wana nafasi kubwa kucheza Ulaya," alisema baba huyo wa watoto wawili walio Serbia.
Lupopo walipanga kuja nchini mwishoni mwa wiki kufanya mazungumzo na Yanga ili kumsajili Nurdin Bakari na Chuji.
Katibu wa Lupopo, Ilunga Lumbala alipotafutwa jana kwenye simu alikuwa bize kwenye kikao na akawa anajibu "Nitafute baadaye jioni nipo kwenye kikao kizito cha kamati."
Nurdin Bakari alisema jana Jumatatu kuwa: "Hii ndio kazi yangu iwapo nitapata mkataba mzuri wa kwenda Lupopo nipo tayari hata sasa."
Wakati Lupopo ikiwataka wachezaji hao wawili, TP Mazembe inawataka Shadrack Nsajigwa, Amir Maftah na Obren Curkovic.