MSHAMBULIAJI wa Simba, Mussa Mgosi ambaye anaamini Arsenal inaweza kuwa bingwa wa England msimu huu amesema huu ni mwaka wa Simba kwenye michuano ya kimataifa.
Mgosi ambaye anaongoza msimamo wa wafungaji kwa mabao 14 mkononi, aliiambia Mwanaspoti kuwa wana mambo mawili tu sasa kukamilisha hesabu za ubingwa wa Bara na kuchunga wasipoteze mechi hata moja pamoja na kufanya kweli Kombe la Shirikisho.
"Tunachotaka sasa ni kuifunga Azam tukamilishe hesabu za ubingwa wa Tanzania pamoja na kuhakikisha kwamba hatupotezi mchezo wowote mpaka msimu unamalizika iwe kwa Yanga au timu yoyote ile inayokuja mbele yetu,"alisema Mgosi ambaye ni baba wa watoto wawili.
"Nadhani pia huu ni mwaka wetu kwenye Kombe la Shirikisho tumepania kufanya kweli kama ilivyokuwa miaka ya nyuma tunataka kuandika rekodi mpya ambayo inawezekana kabisa, hakuna kikwazo,"alisema Mgosi ambaye timu anayoishabikia ya Arsenal ina pointi 61.
Alisema kuna asilimia nyingi kwa Arsenal kutwaa ubingwa msimu huu kama Simba.
"Nikiangalia kila kitu kipo wazi, sisi tunachofanya ni kupangua mechi moja baada ya nyingine kocha wetu tunamuamini na tunajua kwamba ameweka mikakati mizito sana kwa hao Wazimbabwe na tutafanikiwa.
"Kila mechi tunaiwekea mikakati yake mahususi, hatuogopi mtu yoyote tunachofanya ni kufanya maandalizi kulingana na watu tunaocheza nao. Kwenye ufungaji bora simhofii Mrisho Ngassa wala John Boko kama riziki ni yangu ni yangu tu kama ni mwingine ni mambo ya Mungu hayo." Ngassa na Boko wana mabao 12 kila mmoja.