Sep 9, 2010, 9:38 am TFF UEFA FIFA Yahoo Sport CAF Staff Mail Premier League English News Spoti Majuu
 
 
 
 
 
 
 
 

 

Imewekwa:: 2010-03-08 17:45:00
Raha ya ndoa ni huba
Na Dismas Lyassa

TAFITI tofauti zilizofanywa duniani kuhusu maisha zinaeleza kuwa ni muhimu watu wanapofikia umri fulani kuoana.

Zipo sababu nyingi za watafiti kushawishi watu kuoana, lakini mojawapo ya msingi ni kwamba wenye ndoa nzuri mara nyingi huishi maisha marefu zaidi, huwa na afya njema zaidi, kuliko wale wasio kwenye ndoa.

Mwenzi wako ni msaidizi katika maisha yako ya kila siku, unapokuwa na jambo la kuzungumza, ni kwamba tayari unakuwa unaye mtu wa kuzungumza naye.

Watafiti hawa wanaamini ndoa ni jambo la msingi kwa imani kwamba katika ndoa ikiwa kwa mfano mmoja anaumwa, mwenzi wake anaweza kumsaidia kupunguza maumivu kwa kucheza naye hapa na pale.

Kwa ujumla nakubaliana nao, lakini tatizo lililoko ni kwamba ndoa nyingi si za kuvutia hata kidogo. Ni zaidi ya asilimia 70 ya ndoa hazivutii kuigwa hata kidogo.

Je, wewe uko kwenye ndoa? Je, ni kweli mnavyoishi, ndivyo mlivyokuwa mkiishi wakati ule wa uchumba kwa amani na furaha? Mnaandikiana meseji nzuri za kuvutia kama wakati ule? Hebu kumbuka, mko wapi, mlikuwa wapi na ni wapi mnakoenda? Ndoa yako inafaa kuigwa? Jibu unalo.

Wakati fulani ni vizuri kuishi bila mke wala mume, kuliko kuingia kwenye ndoa, ambayo haina maelewano mazuri.

Ikiwa unataka kuingia kwenye ndoa, lakini unaona kasoro za hapa na pale za kitabia ni muhimu kusita kwanza, waza kwa makini kama kweli mtu huyo anakufaa. Usikubali kuendelea na mipango ya kuoana na fulani, wakati umeona ana kasoro, hiyo ndoa huko mbele itakuwa ni hatari. Dalili za mvua ni manyunyu.

Katika suala la ndoa oa au olewa pasipo shinikizo au maneno ya watu…eeh bwana maana katika familia zingine labda binti ana umri fulani hajaolewa wanaanza kumuuliza ‘utaolewa lini’…Ni swali zuri, lakini ni jambo baya, kwa sababu ni kama vile unataka aolewe, bila kujua nini anawaza.

Acha mtu aamue mwenyewe, anataka kuolewa lini, anataka kuolewa na nani. Au kama ni mwanaume acha aamue anataka kuoa lini na anataka kumuoa nani. Ni muhimu sana katika maisha mtu mwenyewe kuwa na maamuzi, pasipo shurutisho.

Kimsingi ni jambo muhimu kwa mwanaume kuoa pale muda unapowadia, lakini ni muhimu zaidi kuwa makini katika kuchagua mtu wa kuoana naye.

Wakati mwingine ni bora kukaa bila ndoa, kuliko kuoa au kuolewa, hii ni kwa sababu kuna baadhi ya watu unapokuwa nao katika maisha hawakupi raha.

Inawezekana wewe ukawa ni mtu mzuri, lakini ambaye unaye ni mbaya, ndivyo inavyotokea kwa baadhi ya ndoa, hali inayosababisha baadhi ya wanandoa kujuta kwa nini walikubali kuoana.

Kitaalam ni kweli ukiwa kwenye ndoa afya yako inakuwa nzuri, lakini ikiwa ndoa hiyo si nzuri, afya huwa mbaya zaidi, msongo wa mawazo huongezeka, kwa ujumla mwenye ndoa mbaya, ana hali ngumu zaidi ya maisha kuliko yule, ambaye yuko huru pasipo ndoa.

Raha mojawapo ya kuoana ni kujaliana, mwenzio akisema naumwa kichwa, unamshika na kumuuliza wapi? …Eee bwana mnataniana, mnafurahiana, kiasi kwamba kitu kidogo kilichokuwa kikisumbua katika ndoa au maisha yako inakwisha.

Raha ya kuingia kwenye ndoa ni kwamba ukiumwa mwenzi wako anakuonea huruma, anakuuliza kama umekunywa dawa nk, lakini kwa mtu ambaye yuko pekee, kila jambo ni lazima alifanye yeye, bila kumtegemea mtu mwingine hasa yale yanayohusu nyumba yake.

Katika ndoa pia kama umempata mwenzi ambaye ni mzuri, mwenzi ambaye pengine ana ujuzi zaidi wa hili na lile kuliko wewe, inakuwa rahisi kupata ujuzi au maarifa hayo kutoka kwake.

Ndoa nzuri ni ile ambayo watu wake wanaheshimiana, watu wake wanakubaliana katika hili na lile. Katika vitabu mbalimbali vya dini vimezungumza kwa kina kuhusu suala hili. Mfano katika Biblia inasema kwamba Adam aliumbwa kutoka kwa vumbi, mchanga ambao haukulainishwa, lakini Hawa aliumbwa kutoka ubavuni mwa mumewe mwenyewe, hakutoka mguuni apate kukanyagwa, wala kichwani apate kumtawala mumewe, bali kutoka ubavuni apate kuwa msaidizi wake, anayefanana naye, anayemfaa.

Je uliyenaye anakufaa? Ni swali la msingi. Lakini ikiwa hakufai, dawa sio kuachana, bali yawapasa kuzungumza kwa kina, ili lile linalowasumbua liondoke, na wakati mwingine si mbaya kutafuta wataalam kaeni nao kuzungumza kuhusu ndoa, kumbuka katika ulimwengu huu kila mtu na kipawa chake, wengine ni mafundi wa magari, wengine ni mafundi wa kushauri, nk.

Wengine wanapokuwa kwenye ndoa zenye kero wanafikiria kuachana, kwa waislam hiyo inawezekana, lakini kwa wakristo kuna ugumu maana imeandikwa “Mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja, basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu hawezi kukitenganisha."

Hii ina maana kuwa yakupasa kuwa makini sana kabla ya kuingia kwenye ndoa, ni hatari na kwa kiasi Fulani ni aibu kuingia katika TALAKA, jihadhari!!!
Toa Maoni Chapisha(Print) Facebook Tuma kwa rafiki
Habari Zingine
Phiri hana shida, Mgosi, Kanoni waibukia Tanga
Mkenya aipa Simba mambo mawili
Henry arudi Norway majeruhi
Kiungo Yanga mambo mazuri
Mafisango atunisha msuli,aigunia Simba Tanga
Humoud azua tafrani Simba
Wabongo wamrudisha Mariga Dar
Rage aidai Mwanaspoti Sh. bilioni moja
Jabulani kumi zaisisimua Simba
Kipa Yanga aingilia anga za Kaseja
 
 
 
 
 
© Mwananchi Communications Ltd:2007-2010:Started October 1,2007http://www.mwanaspoti.co.tz/readnewzt_sp.php?id=3631