FIKRA za wachezaji wa Yanga kama Mrisho Ngassa na Jerry Tegete kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2010, licha ya kiwango cha hali ya juu walichoonyesha kwenye Uwanja wa Stade de Kenya zimeyeyuka.
Yanga ilichapwa bao 1-0 ugenini ambalo pamoja na kipigo cha mabao 3-2 jijini Dar es Salaam ikawa imeaga mashindano kwa idadi ya mabao 4-2. Hali hiyo ilionekana kumkera Kocha Mserbia Kosta Papic ingawa sababu kuu nne ndio zilizoitoa timu yake kwenye mashindano hayo makubwa Afrika.
Kwanza, uzembe wa mabeki uliosababisha kipigo cha mabao 3-2 jijini Dar es Salaam ambacho kiliwapa nguvu kubwa Lupopo kwani mechi ya marudiano walikuwa kwenye uwanja wao ambao hupata sapoti kubwa ya klabu zote za Ligi Kuu Congo ikiwamo TP Mazembe ambao ndio wapinzani wao wakubwa.
Yanga ilihitaji ushindi wa mabao 2-0 ambao uliwawia vigumu ingawa walionyesha jitihada kubwa hasa kwenye safu ya kiungo na ulinzi ambako beki mrefu Mkenya anayekaa benchi kila mara George Owino alionyesha kiwango cha juu kwa kushirikiana na Nadir Haroub 'Cannavaro'.
"Nilimwambia Owino ahakikishe yule jezi namba 9 (Mumba Felix Sunzu) haleti madhara kama ilivyokuwa Dar es Salaam na akaweza kumdhibiti, hakuwa na lolote,"kocha Kosta Papic aliiambia Mwanaspoti ambalo ndio gazeti pekee la Tanzania lililokuwa nchini humo kufuatilia habari za mechi hiyo.
Hata kipa Obren Cuckovic alionyesha kiwango cha juu kwa kuokoa hatari nyingi huku mashabiki wakidai kuwa angesimama langoni mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam Yanga isingekumbana na kipigo kikubwa kama ilivyokuwa kwa Mghana Yaw Berko.
Pili, Yanga ilionyesha dhahiri kwamba inahitaji mshambuliaji mmoja mwenye nguvu na uwezo mkubwa wa kutumbukiza mabao. Aina ya uchezaji wa Nurdin Bakari, Mrisho Ngassa na Jerry Tegete waliokuwa wakiongoza mashambulizi ulionyesha dhahiri kuwa Yanga inahitaji mshambuliaji mmoja mwenye uzoefu na anayeziona nyavu.
Wachezaji hao walipata nafasi nyingi lakini wakaonekana kukosa maarifa ya kutosha kupenya ngome ya Lupopo ingawa waliisumbua mara kadhaa na kupiga mashuti ambayo au yalikuwa hafifu, yalipaa ama kuondoshwa na ukuta mzito uliosukwa na kocha Boualem Mankour.
Tatu, uchafu wa Uwanja wa Stade de Kenya. Uwanja huo unaobeba mashabiki 40,000 uliwaponza wachezaji wengi wa Yanga hususani Nadir Cannavaro, Ngassa, Tegete, Athuman Iddi ambao walionekana kuanguka mara nyingi na kuchafuka matope mwili mzima hadi rangi za jezi zikawa hazionekani.
Mvua kubwa ilinyesha eneo la uwanja na umbali kama wa kilomita mbili kuzunguka eneo hilo la mtaa wa Kenya na kusababisha maji kujaa kwenye sehemu ya kuchezea hali iliyofanya wachezaji wengi kuanguka kila mara na kupoteza ladha ya mchezo.
Licha ya kuvalia viatu vyenye meno mazuri kutokana na kuonywa kabla na Watanzania wanaoishi jijini humo waliokuwa wakifika kila mara kwenye hotel ya de la Rose haikusaidia kwani mara nyingi hususani walipokuwa wakipanga mashambulizi Yanga walikuwa wakiteleza na kupoteza mipira.
Uongozi wa uwanja uliondoa maji uwanjani lakini bado yakaonekana kutuama vikundi vikundi katika sehemu zilizokuwa na upara katikati ya uwanja. Hali hiyo ilimfurahisha kocha Boualem Mankour kwani hakuamini kama angeenda mapumziko bila kuifunga Yanga.
"Nilipoona tumekwenda mapumziko nilikuwa sina raha kwavile Yanga walikuwa vizuri na nilijua wangebadili matokeo ya mchezo ila hali ya uwanja imewavuruga ufundi wao ukapotea,"anasema.
"Majimaji na matope yaliyosababishwa na ile mvua kubwa yalisaidia sana mimi kushinda kwavile wachezaji wangu wamezoea hiyo hali, kama kusingekuwa na hali ya mvua matokeo yangebadilika sana halafu na ushindi wa Dar es Salaam umetusaidia pamoja na sapoti ya mashabiki."
Nne, Sapoti kubwa ya Serikali ya Jimbo la Katanga ilipo Lubumbashi pamoja na mshikamano wa mashabiki wa FC Lupopo na TP Mazembe ambao kwenye mechi za ligi wamekuwa wapinzani wakubwa pengine kushinda Simba na Yanga.
Gavana wa Jimbo la Katanga, Mosses Katumbi ambaye ni Rais wa Mazembe alikuwa akitangaza kuanzia siku moja kabla na siku yenyewe ya mchezo kupitia redio za Mwangaza na Nyota kuomba mashabiki wa Mazembe waisaidie Lupopo iifunge Yanga na kweli ikawa hivyo uwanjani.
Katumbi aliingia uwanjani na kuibua hamasa kubwa na kelele uwanja mzima kuizomea Yanga na kuishangilia Lupopo ambapo mpaka mashabiki wa Yanga waliokwenda na gari aina ya Coaster wakanywea kwavile walikuwa hawasikiki.
Redio za Lubumbashi zilihamasisha mashabiki tangu asubuhi mpaka muda wa mchezo, ambapo kiongozi wa vikundi vya mashabiki wa Mazembe alisikika akisema kuwa ; "Tumevamiwa na adui Yanga tumshambulie aondoke halafu tuendelee na mambo yetu." Mashabiki wote walimtii na kuvaa jezi za Lupopo za rangi ya njano.
Kelele hizo na muungano wa mashabiki uliwashangaza wachezaji wa Yanga huku Boniface Ambani akitamani mashabiki wa Simba na Yanga wangemwagwa uwanjani hapo ghafla na kushuhudia hali hiyo.
Kwa mujibu wa Papic nyota wa mechi hizo mbili nyumbani na ugenini ni kiungo Athuman Iddi: "Tumetolewa kwenye mashindano baada ya kupoteza mechi ya Dar es Salaam si hapa Lubumbashi, hii imechangia sehemu ndogo sana angalia na kiwango cha hapa ni cha juu sana, Lupopo wamepata bao lakini hawajafanya cha ajabu, tumewakamata tumeshindwa kutumia nafasi."
"Halafu uwanja mbovu sana maji kila sehemu wachezaji wanaanguka tu kila mara,"anasema Papic huku Mwenyekiti wa timu hiyo iliyofikia kwenye hoteli ya mmiliki wa Lupopo, Imani Madega akiwaambia mashabiki "tugange yajayo hakuna la kufanya."