MWANAMITINDO, Naomi Campbell huenda akaingia katika vita na polisi baada ya kudaiwa kumfanyia fujo dereva wake, jijini New York.
Campbell, mwenye miaka 39, alitakiwa kufika polisi kutoa maelezo baada ya kumnasa kibao dereva wake majira ya saa 9:00 alasiri, Jumanne wiki hii.
Imefahamika kuwa baada ya tukio hilo Naomi alitoka nje ya gari na kuchukua usafiri mwingine.
Baada ya hapo dereva huyo alifika polisi na kushitaki.
Lakini msemaji wa mwanamitindo huyo alieleza: "Nadhani hukumu haitatolewa haraka, uchunguzi utafanyika. Kuna mambo mengine zaidi ya kibao hicho."
Hiyo si mara ya kwanza kwa Naomi kumfanyia fujo mfanyakazi wake, mwaka 2006 alimpiga mfanyakazi wake wa ndani na baadaye alihukumiwa kufanya kazi za jamii.
Na katika tukio jingine, mwaka 2007, Naomi alihukumiwa kufanya kazi za jamii kwa saa 200 baada ya kupatikana na hatia ya kuwatusi polisi.