MWAKA jana timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars ilichapwa mabao 2-0 na timu ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) katika pambano la kimataifa la kirafiki lililofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Wataalamu wetu wa kukosoa walikimbilia katika vituo vya televisheni na redio kuelezea ubovu wa Stars. Wakabwabwaja kadri walivyoweza na tukawasikia.
Juzi klabu ya FC Lupopo ya DRC ilikuwa kazini ikiwathibitishia wachambuzi wetu kwamba soka la Tanzania huwezi kulilinganisha na wenzetu kwa kukimbilia katika vyombo vya habari na kusema ovyo.
Lupopo imeiondoa Yanga kwa jumla ya mabao 4-2 na kwa wasiofahamu, Lupopo sio mabingwa wa DRC. Inashiriki michuano hiyo kwa sababu nchi hiyo ina nafasi zaidi ya moja katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na kufanya vema katika michuano hiyo.
Tatizo la soka letu ni siasa. Badala ya kucheza mpira na kufanya maandalizi wengi wetu tunacheza siasa. Hatuwezi kupata Stars iliyo imara kwa kukimbilia katika vyombo vya habari na kulaumu.
Kwa nchi kama yetu ambayo haina wanaocheza nje ya nchi basi ni lazima klabu ziwajibike kuandaa wachezaji.
Klabu zetu za Simba na Yanga zina kawaida ya kutolewa mapema kwenye michuano ya Afrika. Ni vipi wachezaji hawa wanabadili matokeo kwa urahisi pindi wanapoichezea timu ya taifa?
Yanga ina wachezaji saba katika timu ya taifa na wengi kati yao ni tegemeo. Kama Yanga inachapwa 4-2 na Lupopo (Si TP Mazembe), inawezekana vipi Stars kuichapa DRC 3-0 hata kama wenzetu wanatumia wachezaji wao wa ndani?
Jiulize, ni kwa nini DRC ilitwaa michuano ya CHAN? Kwa sababu ndani ya nchi yao kuna klabu mahiri ambazo zinashindana katika michuano ya Afrika na si kushiriki. Wakati Congo wakitwaa CHAN, Mazembe imekuwa bingwa wa Afrika. Hivi hatuoni kwamba kuna mlinganisho ulio wazi wa mafanikio baina ya klabu na nchi?.
Huu ni wakati muafaka kwa wachambuzi wetu mahiri wa kukimbilia kwenye redio na kuanza kufanya hivyo kwa matokeo mabovu ya klabu zetu kama ilivyotokea kwa Yanga.
Katika mfumo wa soka letu usio na wachezaji mahiri wa kulipwa nje ni vigumu kupata Stars imara huku Yanga na Simba zikiishia raundi ya kwanza ya michuano ya Afrika. Ni kujidanganya.
Mbio zetu za kutafuta simu za akina Maulid Kitenge wa Redio One zisiishie kwa matokeo mabovu ya Stars halafu tukasahau matokeo ya Yanga. Wachezaji wanaoiwakilisha Stars ni wale wale wanaoziwakilisha Simba na Yanga katika michuano ya kimataifa. Hakuna miujiza.
Tusipojua tulipokwama kamwe hatuwezi kujua tena kufanikiwa. Tufanye kazi ngumu kuanzia ngazi ya klabu na soka la vijana. Stars si sehemu ya mchezaji kufundishwa mpira, wachambuzi wetu waelewe hili.
Stars ikifungwa 5-0 na Nigeria watu tutalaumu, wakati Simba ikifungwa jumla ya mabao 7-3 na Enyimba watu tunakaa kimya. Hatuoni kuwa kuna uhusiano hapo na hasa kwa nchi yetu ambayo wachezaji wa timu ya taifa wanacheza nyumbani?