JOPO la Yanga chini ya Kocha Mkuu, Kostadin Papic limevania Lubumbashi ilipopiga kambi Saint FC Lupopo wanayocheza nayo Jumamosi ijayo kwenye mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa jijini Dar es Salaam.
Papic atapa nafasi ya kuwashuhudia wachezaji kama Ndume wa Ndume, Felicien Kabundi, Nsumbu Ditwabanza na Mutiu Adegoke ambao kwa mujibu wa mitandao ya habari ya nchi hiyo ni miongoni mwa vifaa tegemeo.
Kocha aliondoka jijini Dar es Salaam peke yake jana Ijumaa alfajiri kwa ndege ya Shirika la Kenya kupitia Nairobi na usiku wa kuamkia leo alitazamiwa kulala jijini Kinshasa.
Kwa mujibu wa viongozi wa Yanga Papic alitazamiwa kupokewa na jopo na Watanzania wanaoishi Kinshasa ambao ni mashabiki wa Jangwani na leo atakwenda Lubumbashi kwenye Uwanja wa Frederick Kibassa Maliba unaobeba watu 35,000 kuiona Lupopo.
"Kocha ameondoka alfajiri sana na ndege ya KQ kwenda DR Congo kuiona Lupopo na atarudi Dar es Salaam Jumapili, tayari kwa mechi ya Jumatatu dhidi ya Mtibwa,"Kiongozi mmoja wa Yanga aliiambia Mwanaspoti jana.
Lupopo chini ya Kocha Mualgeria, Boualem Mankour ipo kwenye kundi D la ligi ya DRC na imeshinda mechi zote tatu ilizocheza tangu ligi ianze wikichache zilizopita.
Papic aliyewahi kuzinoa Kaizer Chiefs na Orlando Pirates za Afrika Kusini aliiambia Mwanaspoti jijini Dar es Salaam juzi kwamba ataishangaza Lupopo na Africa kwa ujumla katika mechi hiyo ya Jumapili kwavile wataka kuonyesha kuwa wanaweza na wao ndio Yanga.
"Mambo yanakwenda vizuri tunajitahidi kwa kila hali kadri inavyowezekana kuhakikisha kwamba tunaanza vizuri mechi yetu na Lupopo, tunajua ni timu ngumu lakini tunataka kuwaonyesha."
"Tunataka kuwathibitishia na kuwaonyesha kwamba uwezo tunao wa kupambana na wachezaji wetu wana viwango vya kupambana na mtu yoyote yule katika mazingira.
"Tutawaonyesha ubora wetu kwa kuwachezea mpira na kupata matokeo mazuri ambayo yataturahisishia mechi ya marudiano.
"Kwa mwenendo ninaouona kwa wachezaji naamini kwamba hakuna kisichowezekana, wanaweza kuwashangaza na kufanya kazi nzuri soka inachezwa kwa uwazi na ninachoweza kusema ni kuwa tutawashangaza."
Bosi huyo maarufu kama Clinton awali aliuomba uongozi umtafutie mechi mbili za nje ya nchi kabla ya kucheza na Lupopo pamoja na kumtafutia visa aende DRC kuangalia ligi ya huko lakini uongozi umemuambia suala la kucheza mechi nje ni mpaka mechi ya marudiano.