Na Mwandishi Wetu
FC Lupopo inayocheza na Yanga kwenye mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Jumamosi ijayo jijini Dar es Salaam imezidi kupepea katika msimamo wa ligi wa DR Congo.
Timu hiyo ni kati ya vigogo vya soka DRC ikiwa imewahi kunyakua ubingwa mara saba katika miaka ya 1958, 1968, 1981, 1986, 1990, 2002 na 2009.
Lupopo iliyopo kundi D lililopo Lubumbashi inaongoza kwa pointi tisa baada ya kushinda mechi zake tatu ambazo tangu ligi kuu msimu wa 2010 ianze Januari 27.
Katika mechi ya kwanza timu hiyo ilishinda bao 1-0 dhidi ya JS de Likasi, ikaifunga Bantous mabao 5-0 Januari 31 na juzi Jumatano ikaikung'uta tena JS de Likasi mabao 2-0 katika mechi ya marudiano.
Ligi ya DRC inaendeshwa kwa mfumo wa majimbo ambapo timu 28 zimegawanywa katika vituo sita ambavyo ni Goma, Kinshasa, Kisangani, Matadi, Mbuji-Mayi na Lubumbashi ilipo Lupopo ya Yanga.