HENRY Joseph anayeichezea Kongsvinger ya Norway amesema kuwa yupo fiti tayari kwa Ligi Kuu ya nchi hiyo inayoanza mwezi Machi.
Mchezaji huyo wa zamani wa Simba aliiambia Mwanaspoti kwa njia ya simu jana kuwa kila kitu kinaenda safi na ameshakuwa fiti asilimia mia moja.
"Nafanya mazoezi sana na maumivu ya mbavu yaliyokuwa yananikabili yameshakwisha kama wiki mbili au tatu zilizopita na madaktari wamesema niko salama kwa shughuli,"alisema Henry aliyezaliwa miaka 25 iliyopita jijini Mwanza, Tanzania.
"Sasa hivi najinoa sana nataka niwe fiti kwa mechi za kirafiki ambazo zinaanza wiki ijayo na Ligi Kuu ambayo inakuja siku za usoni.
"Ninavyojiona niko vizuri sana na nitafanya vizuri sana kadri inavyowezekana kama sitaumia tena wala kusumbuliwa na tatizo lolote," ambaye, aliibuliwa na Simba kutoka kwenye shule ya sekondari ya Makongo.
Henry aliumia mbavu katika mechi ya kirafiki kwenye uwanja wa Taifa baina ya Taifa Stars na Ivory Coast. Stars ilifungwa bao 1-0 na Didier Drogba anayeichezea Chelsea ya England, ambayo kesho Jumapili inacheza na Arsenal.