BEKI wa kati wa Kagera Sugar wa hapa, Said Morad amesema mshambuliaji wa Simba Mussa Mgosi alishindwa kuwafunga kutokana na kujigamba mno katika vyombo vya habari.
Morad alitolea pia mfano wa Boniface Ambani wa Yanga ambaye msimu uliopita alijigamba kuwa angetangazia ubingwa Kaitaba kibao kikamgeukia timu yake ikapoteza.
"Najua aina ya uchezaji wake kwamba ni wa kasi na nguvu na akikupita umeumia ndio maana nikala naye sambamba,"alisema Morad ambaye amewahi kuichezea Simba,Manyema na Ashanti.
Mchezaji huyo ambaye mwaka juzi alikuwa kwenye kikosi cha Kilimanjaro Stars kilichoshiriki Chalenji nchini Ethiopia, alisema walitengeneza mkakati na kukubaliana naye na bora kufungwa na mchezaji mwingine lakini si Mgosi.
Morad ambaye anavutiwa na uchezaji wa beki wa kati wa Manchester United Rio Ferdinand, alisema "Mimi nafanya mazoezi na mshambuliaji hatari wa Kagera, Shija Mkina yupo na sifa kama za Mgosi kwa hiyo ilikuwa rahisi."
"Unaweza kuona hata bao walilotufunga lilikuwa la adhabu,walishindwa kutufunga kwa njia za kawaida."
"Hata mechi ya Yanga Dar es Salaam hao kina Ambani, Jerry Tegete tutawazuia hivi hivi na hawataamini, wote wanakabika."