BONDIA wa Tanzania, Francis Cheka, amesema kuwa hawezi kucheza pambano lake dhidi ya Bondia Stephen Chungu wa Zambia kutokana na kupata ofa ya pambano lingine.
Cheka alipangwa kupambana na Chungu mwezi ujao jijini, lakini amesema kwa sasa ana mazungumzo na promota mwingine ili apambane na bondia mmoja maarufu kupitia chama kingine.
Bondia huyo aliiambia Mwanaspoti, kuwa ameamua kutocheza pambano hilo kwani anatarajia kucheza pambano jingine ambalo anaamini litakuwa na dau kubwa.
Alisema kuwa atakuwa tayari kucheza pambano hilo na kutetea ubingwa huo, ambao anaendelea kuushikilia hapo mwezi Mei, mwaka huu.
"Nimeamua kutocheza pambano hilo kwani natarajia kuwa na pambano lingine ambalo litakuwa na dau kubwa hivyo kupanga kucheza pambano hilo mwezi wa tano, ingawa kwa kipindi hiki nitakuwa katika mazoezi ya kawaida," alieleza Cheka, ambaye ametokea tishio nchini kutokana na kuwadunda mabondia maarufu kama Rashid Matumla na Joseph Kaseba.
Mbali na Cheka ambaye amejitoa, siku hiyo bondia Mbwana Matumla atatetea ubingwa wake wa mabara wa UBO wa uzito wa bantam dhidi ya bondia kutoka Uganda, Sunday Kizito.
Mbwana alitetea ubingwa wake huo kwa kumchapa bondia kutoka Uganda, Festus Omondi katika raundi ya tano katika pambano lililofanyika kwenye ukumbi wa PTA.
Pambano hilo limeandaliwa na kampuni ya Prime Time Promotions chini ya promota, Joseph Kusaga na litakuwa la raundi 12.
Matumla kwa sasa ameshinda mapambano 19 ambapo 11 ni kwa KO, amepigwa manne, mawili kwa KO wakati Kizito ameshinda mapambano 10, matano kwa KO, amepoteza manane na moja kwa KO.