KOCHA mkuu wa timu ya Toto Africa, Choke Abeid amesema licha ya kufufua matumaini ya kutoshuka daraja bado anahitaji kushinda mechi zake zote za nyumbani.
Timu hiyo imebakisha mechi tano itakazocheza nyumbani katika uwanja wa CCM Kirumba dhidi ya African Lyon, Kagera Sugar, JKT Ruvu, Mtibwa Sugar pamoja na Prisons.
"Tunahitaji kufanya vizuri katika mechi zote tano za nyumbani zilizobakia lakini pia tukijitahidi kadri ya uwezo wetu wote kuhakikisha hatupotezi mechi za ugenini."
"Ushindi tuliyoupata kwa Manyema umefufua matumaini yetu ya kufanya vizuri katika mechi zetu zote zilizobakia hivyo nawaomba wapenzi na mashabiki wa timu yetu waendeleze mshikamano," ambaye alikuwa kiungo tegemeo wa Pamba ya Mwanza wakati iliposhika nafasi ya pili kwenye ligi ya Tanzania Bara mwaka 1984.
Ushindi wa Toto African wa mabao 4-2 dhidi ya Manyema ni ushindi wa pili kwa timu hiyo tangu ilipoanza mikikimikiki ya Ligi Kuu msimu huu baada ya ule wa Kagera Sugar.
Timu hiyo itacheza Februari 13 dhidi ya African Lyon katika mchezo wake wa 16 utakaofanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.