Sep 9, 2010, 9:13 am TFF UEFA FIFA Yahoo Sport CAF Staff Mail Premier League English News Spoti Majuu
 
 
 
 
 
 
 
 

 

Imewekwa:: 2010-02-01 18:51:00
Unaijua Simba kuliko mimi, halafu?
Nahodha wa Simba,Nico Nyagawa
Na Edo Kumwembe
TAJIRI wa Kirusi Roman Abramovich alizaliwa Oktoba 24, 1966. Ilikuwa ni miaka 61 baada ya kuanzishwa kwa klabu anayoimiliki ya Chelsea iliyopo jiji la London.

Kabla Roman hajazaliwa, miaka 11 iliyopita Chelsea ilikuwa inatwaa taji lake la kwanza la Ligi ya England. Hii ilikuwa katika msimu wa mwaka 1954/55.

Niliikuwa najikumbusha historia hii wiki iliyopita baada ya kukuta makomandoo fulani wa soka nje ya Uwanja wa Taifa wakijisifu namna wanavyozifahamu klabu za Simba na Yanga.

Mmoja ambaye alikuwa na umri wa makamo alionekana kujinadi kuwa yeye alikuwa anaifahamu Simba kuliko mtu yoyote katika kundi hilo. Mwishowe akajinadi jinsi alivyokuwa rafiki kipenzi wa winga wa zamani wa Simba, marehemu Willy Mwaijibe.

Mwingine wa Yanga akaibuka akielezea namna anavyoifahamu Yanga kwa undani. Akaelezea namna alivyoshuhudia pambano la mwaka 1969 kati ya Simba na Yanga lililochezwa uwanja wa Karume.

Wote walionekana kutembea vifua wazi na mwishowe wakaingiza siasa hizi katika chaguzi za klabu zao na mwisho hawakuonekana kujadili maendeleo ya klabu zao. Watu kama hawa wanajisifu kuwa bila ya wao hakuna klabu.

Huu ni ujinga uliotutawala. Watu wanashindwa kujadili mawazo mapya na hisia mpya huku wakiruhusu watu wapya waingie katika klabu zao kwa kisingizo cha kuzijua sana klabu hizi kuliko wengine.

Kuna sifa gani ya kujifanya unaifahamu vema Simba wakati jengo lake ni miongoni mwa majengo chakavu zaidi katika mtaa wa Msimbazi kama si eneo la Kariakoo kwa ujumla? Historia inatusaidia nini wakati unakwamisha maendeleo ya klabu kwa kisingizo cha kuifahamu vema?

Mtu anajisifu anaifahamu vema Yanga mpaka povu linamtoka mdomoni, lakini hatuambii alikuwa wapi wakati jengo lilipochakaa mpaka alipojitokeza Mdhamini Yusuf Manji kulikarabati kwa fedha zake za mfukoni.

Mtu mwenye hisia za maendeleo na mipango mipya anaweza asisikilizwe lolote kwa sababu ataambiwa haifahamu Yanga na hakuwa amezaliwa wakati Yanga ikiichapa Simba 2-1 pale Nyamagana mwaka 1974.

Hivi ilikuwa ni lazima wote tuzaliwe mapema kwa ajili ya kushuhudia kuzaliwa kwa Simba na Yanga au historia zao za zamani?

Kuna vijana wamezaliwa mwishoni mwa miaka ya 1970 na mwanzoni mwa miaka ya 1980 na leo ndiyo wanaziongoza taasisi kama benki, kampuni za simu, vituo vya Televisheni na idara nyingine kwa mafanikio.

Hawa hawaruhusiwi kuongoza klabu zetu kwa kasi mpya kwa sababu hawakuwepo wakati Simba ikicheza nusu fainali ya klabu bingwa ya Afrika mwaka 1974 dhidi ya Mehallal El Kubra.

Na ndiyo maana nilianza kwa kutoa mfano namna mmiliki wa sasa wa Chelsea, Roman Abramovich alivyoikuta klabu hiyo ikiishi miaka 61 kabla hajazaliwa pale Urusi. Kama Chelsea wangekuwa wanafuata misingi ya siasa za soka letu basi leo Roman angekuwa historia pale Stamford Bridge.

Imefika wakati sasa turuhusu mawazo mapya, nguvu mpya na malengo mapya bila ya kujali ‘uzamani’ ambao hauna maana. Mwanachama au shabiki akiwa kijana au mzee si tija, kitu muhimu zaidi ni kuzingatia hisia zake za kisasa ambazo zitatupa mwanga wa kufikia maendeleo ya Kaizer Chiefs.

Kuna haja gani ya kujisifia sana kwamba unaifahamu Simba au Yanga tangu mwaka 1950 wakati Kaizer Chief ya Afrika Kusini iliyoanzishwa mwaka 1970 ni klabu tajiri mara sabini kuliko klabu zetu kongwe?

Kuna haja gani ya kujisifia kuwa bila ya wewe hakuna anayeweza kuongoza Simba au Yanga wakati hata ukituchagulia viongozi hawawezi kutupatia mabasi ya timu kama ilivyo kwa Azam FC.

Unajisifia unaifahamu sana Simba kuliko mimi, halafu iweje? Kama umeshindwa kuisaidia Simba basi unaweza kukaa kando na mimi mwenye mawazo mapya na ya kisasa nikaifikisha Simba mbali kuliko wewe ulikoitoa.

Marehemu Tabu Mangara ambaye alisaidia upatikanaji wa jengo la Yanga hata akiamka leo basi nitaufumba mdomo. Huyu hana tofauti sana na wazee marehemu waliopata wazo na kuujenga uwanja wa Old Trafford ambao Manchester United mpaka leo wanauchezea.

Lakini kama tunabaki kusimulia historia nyingi za zamani bila ya tija basi haina maana. Historia yako ya kufahamiana na Mwaijibe haina maana sana kama ulishindwa kuipatia Simba uwanja wake binafsi wa mazoezi.

Kama kuna kijana mwenye miaka 25 ana uwezo na mbinu za kuipatia Simba uwanja wake binafsi wa mazoezi basi litakuwa jambo la maana zaidi kuliko kutusimulia jinsi ambavyo ulikuwa rafiki wa karibu na Mwaijibe.

Chaguzi zetu zinatuletea viongozi wabovu kwa sababu hizi. Katiba zetu zinacheleweshwa kubadilishwa kwa sababu hizi. Kuna watu wamejitengezea wigo mdogo na kujifahamu wao wanazijua timu hizi kwa undani kuliko wengine.

Hawataki kufungua milango kwa yoyote mwenye hisia mpya na mbinu za kisasa kuzigeuza Simba na Yanga kuwa klabu za kisasa. Watu wakiingia ubia kuliendesha jengo la klabu na NSSF tutaambiwa tumeuza historia za klabu.

Ebu tujiulize mara mbili. Unaifahamu Simba kuliko mimi, halafu? Unaifahamu Yanga kuliko mimi, halafu? Kuna sifa gani hapo ya maana kama hukuisaidia Simba au Yanga kuwa moja kati ya timu bora barani Afrika?

Hata katika maisha yetu ya kila siku tujiulize. Unajisifu umefanya kazi fulani kwa muda mrefu, halafu? Una nini chako au ambacho umeipatia familia yako?

Lakini kwanza tuanzie kwa wanaojifanya wanazifahamu klabu hizi kwa muda mrefu lakini bila ya tija. Sawa, unaijua Simba kuliko mimi, halafu?

0713 773678
Toa Maoni Chapisha(Print) Facebook Tuma kwa rafiki
Habari Zingine
Phiri hana shida, Mgosi, Kanoni waibukia Tanga
Mkenya aipa Simba mambo mawili
Henry arudi Norway majeruhi
Kiungo Yanga mambo mazuri
Mafisango atunisha msuli,aigunia Simba Tanga
Humoud azua tafrani Simba
Wabongo wamrudisha Mariga Dar
Rage aidai Mwanaspoti Sh. bilioni moja
Jabulani kumi zaisisimua Simba
Kipa Yanga aingilia anga za Kaseja
 
 
 
 
 
© Mwananchi Communications Ltd:2007-2010:Started October 1,2007http://www.mwanaspoti.co.tz/readnewzt_sp.php?id=3469