MSANII mahiri wa filamu, Jacqueline amedai kuwa kuna watu wana wivu na maendeleo yake na ndio waliokuwa wakimgombanisha na Jini Kabula.
Wasanii hao walikuwa na ugomvi mkubwa katika siku za karibuni huku wakiwa hawazungumzi. Lakini ikadaiwa kuwa walikuwa wakigombania na walikuwa wakigombanishwa na prodyuza mmoja.
Lakini Jacqueline alipozungumza na Mwanaspoti wiki hii amesema kuwa mambo hayo wameshayamaliza na wamebaini kuwa kuna watu walikuwa wanawagombanisha kwa masilahi yao.
"Kulikuwa na watu waliokuwa wanafurahia mimi kuwa na ugomvi na Kabula na hao ndiyo walikuwa wachonganishi wetu, baada ya kugundua hilo tukasawazisha tofauti zetu na sasa tunaishi pamoja tena kwa maelewano zaidi," anasema Jacqueline.
"Tulikuwa hatupendani kiasi kwamba kila mtu akimuona mwenzake anaona ni kama vile Paka na Panya, kila mtu anamuona mwenzake ni hatari kama Chui ambapo muda wowote anaweza kumrarua mwenzie.
"Hiyo ni chuki ambayo tulikuwa tukigombanishwa bila kujijua tena na marafiki zetu wa karibu sana, leo naambiwa hivi kesho vile halafu hao hao wanakwenda kwa Kabula na kumwambia maneno kama hayo, hivyo sisi tunaongeza chuki.
"Nawataarifu wale wavimba macho ambao ndiyo walikuwa mamesenja wetu wa kupeleka ujumbe kwa Kabula na kuleta kwangu, kuwa mbinu zao chafu tumezishtukia hivyo waache siyo tabia nzuri, mabinti warembo kama wao kuwa wachonganishi hawapendezi."
Anasema bifu katika maendeleo ya sanaa haswa ya filamu ni kichekesho na haisaidii kuijenga jamii ambayo ndiyo inayowaangalia.
Binti huyo ameongeza kuwa wasanii wengi wa kike wamekuwa hawajiamini ndio maana hujirahisisha kwa maprodyuza.
"Msanii wa kike anatumia muda wake na mbinu zote kuhakikisha anampata prodyuza kimapenzi, anajua kwa kufanya hivyo mambo yake yatakuwa yamenyooka na maisha yatakuwa mazuri kumbe siyo ni upuuzi tu.Sisi wasichana ndiyo chanzo cha kuporomosha sanaa hii na si wao"
"Mwanaume ni binadamu mwenye hisia kama walivyo wengine hivyo kama binti amemtega unategemea nini, sioni sababu ya kuendelea kuwalaumu wakati tatizo la hayo yote ni sisi wasichana kwa kupenda vya dezo vya bila kutoa jasho."
Jacqueline anasema kinachotakiwa ni binti kujilinda na kujua nini anatafuta katika maisha yake; "Tupo ambao tunafanya sanaa hii kama kazi ya kuendesha maisha na wengine wanafanya kujifurahisha na pia wapo wenye sababu zao nyingine."
"Hao sasa ndiyo wanaotuchafulia sanaa hii na kupakaza kashfa kwa kuchafua watu baada ya kuvikosa walivyotarajia kuvipata unakuta mtu alitarajia kuolewa au kupata gari anajikuta akiambulia patupu, sasa zile aibu anaamua kupakaza,"ana msanii huyo.
Jacqueline amezaliwa mwaka 1985 na ni mama wa mtoto moja wa kiume mwenye umri wa miaka minne aitwaye Calix na amepata elimu yake ya msingi katika shule ya Kimara Baruti na baadaye sekondari za Rwandai na Popatial zilizoko Tanga kwa elimu ya juu.
Amewahi kushiriki katika mabango mengi ya matangazo nchini na baadhi ya filam alizowahi kucheza ni 'Oprah', 'Red Valentine', 'Branch of Love', 'Sakata la Mapenzi' na 'Question Mark' hivi sasa yupo kambini kwa maandalizi ya tamthilia ya Millosis na filamu ya 'Beautifull'.