Sep 9, 2010, 9:07 am TFF UEFA FIFA Yahoo Sport CAF Staff Mail Premier League English News Spoti Majuu
 
 
 
 
 
 
 
 

 

Imewekwa:: 2010-01-25 18:37:00
Mnatia aibu
Afande Sele
Na Michael Momburi

AFANDE Sele ametambulisha singo mpya ya 'Kingdom' ambayo inafanya vizuri katika vituo mbalimbali vya muziki jijini Dar es Salaam, lakini amesema wazi kwamba Joh Makini ni mmoja kati ya watu aliowaimba.

Mfalme huyo wa Rhymes anasema kuwa ujumbe uliopo kwenye wimbo huo ameuelekeza wazi kwa msanii huyo kwa madai kuwa anatumia maneno machafu katika nyimbo zake ambayo yanashusha hadhi ya muziki huo.

Msanii huyo ambaye ni shabiki wa Simba, alitolea mfano wimbo wa 'Niaje Nivipi' ambao amedai Makini ametumia maneno ya kudhalilisha wanawake wa nchi masikini kama Tanzania ambao ni mashabiki wa hip hop na Bongo flava.

"Afande amerudi na katika singo yangu nimewaambia wasanii wabadilike, watu wanaimba vitu ambavyo ni aibu mbele ya jamii halafu wanaishia kujisifu kwamba wao ni mabingwa kwenye huu muziki,"anasema msanii huyo ambaye mtoto wake wa kwanza anaitwa Tunda.

"Kwa mfano msanii kama Joh Makini anaimba maneno mengine ambayo ni aibu na yanadhalilisha anasema 'washindi wa tuzo za Kili wanavuja kama fistula halafu anasema tena jipime kama una tundu nyuma ya kaptula' sasa maneno gani haya.

"Si uungwana huku ni kudhalilisha Mama zetu weusi, huu muziki una mashabiki wa aina mbalimbali, hawa wagonjwa wa fistula hawakupenda kuwa hivyo ni mambo ya Mungu hayo. Sasa msanii unavyosimama kwenye kipaza sauti na kuimba maneno kama haya si uungwana.

"Unadhalilisha watu wengine, tusiige mambo ya Kimarekani ambayo hayatufai si kila kitu anachofanya msanii wa Marekani wewe Mtanzania ufanye, tubadilike. Tusidhalilishe mama zetu, halafu cha ajabu kwenye redio madj wanang'ang'ania sana wimbo kama huo na wanaupa chati sana bila kuangalia madhara yake."

"Kama umegombana na watu wa Kili waambie si kutumia maneno makali kiasi hicho, sasa mama zetu waliolala hospitali wakisikia huo wimbo watajisikiaje na watachukuliaje huu muziki."

Afande anasema wimbo wake mpya unazungumza maendeleo ya muziki kwa ujumla na ameongelea upuuzi wa baadhi ya wasanii ambao hawajitambui hali ambayo imefanya muziki kudumaa.

"Unajua wasanii wengi wanaoibuka sasa hawasaidii muziki ukue, huwezi kila siku ukaimba nyimbo za mapenzi tu halafu katika hizo nyimbo hakuna ujumbe wa maana, watu wanabana bana pua tu hakuna cha maana humo ndani.

"We mtoto wa miaka 12 anaimba mapenzi atamfundisha nini mtu hapo? Matokeo yake mtu anakuwa na jina kubwa lakini jamii huku mtaani haimkubali kabisa na nyimbo zake mtu mzima na akili zako huwezi kuzisikiza.

"Watu waimbe ujumbe waige kwa wasanii kama Mrisho Mpoto na wengineo ambao ukiangalia kazi zao zina ubora wa wastani lakini wana ujumbe ndio maana kila siku wanapata dili za maana na wanachukua tuzo.

"Ubora wa muziki si video ya milioni moja, mbona Mpoto anarekodia Uswahilini lakini yuko juu na jamii inakubali ujumbe wake? Jamii nayo ibadilike isikubali wasanii wa ajabu ajabu, mimi kwangu ni bora mara kumi kusikiliza taarab ya Melody 'Mwanamke Hulka' pale kuna watu wanaoweza kunifundisha mapenzi lakini si hawa watoto.

"Jamii isimpende msanii kwavile kabana pua, iangalie kazi ya maana. Huwezi kujiita Rais wa wasanii au Rais wa Manzese wakati unaimba matusi, Rais gani unatukana hovyo, Rais gani huna ofisi? Wewe unajiita Rais lakini unaimba vitu vya kipuuzi ambavyo mtu akisikia anaona kabisa kuwa umekurupuka.

"Hapa natolea mfano wimbo wa Madee alivyoimba eti 'Mfalme gani ana rasta chafu' hapo kwa mtazamo wa haraka alikuwa ananisema mimi lakini mimi nashindwa kumuelewa na ndio maana nakwambia kuwa hawa wasanii hawakustahili kabisa kupewa nafasi.

"Wewe unasema rasta zangu chafu umekuwa Mama Tunda wewe? Yeye ni mke wangu mimi? Na kile alichoimba hata kama ni cha ukweli kinaisaidiaje jamii masikini ya Tanzania, tuimbe vitu vya maana jamii inahitaji kujifunza sana kutoka kwetu wasanii."

Afande anasema kuwa wimbo wake wa 'Kingdom' ni utambulisho na ujio wake mpya na anashukuru kwamba kwa siku chache uliposikika mashabiki wameukubali na lengo lake ni zuri kwa malezi ya jamii mpya ya Kitanzania na muziki kwa ujumla.
Toa Maoni Chapisha(Print) Facebook Tuma kwa rafiki
Habari Zingine
Phiri hana shida, Mgosi, Kanoni waibukia Tanga
Mkenya aipa Simba mambo mawili
Henry arudi Norway majeruhi
Kiungo Yanga mambo mazuri
Mafisango atunisha msuli,aigunia Simba Tanga
Humoud azua tafrani Simba
Wabongo wamrudisha Mariga Dar
Rage aidai Mwanaspoti Sh. bilioni moja
Jabulani kumi zaisisimua Simba
Kipa Yanga aingilia anga za Kaseja
 
 
 
 
 
© Mwananchi Communications Ltd:2007-2010:Started October 1,2007http://www.mwanaspoti.co.tz/readnewzt_sp.php?id=3444