Nilikuwa nimekaa jukwaani katika pambano kati ya Ghana na Morocco mechi za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka juzi jijini Accra, Ghana.
Kikosi cha Ghana kikaingia uwanjani kupasha miili yao moto kikiongozwa na Ally Sulley Muntari. Sikuweza kuamini kilichotokea.
Mashabiki walisimama kwa nguvu zao zote na kuanza kupiga makofi. Muntari akasogea karibu kabisa na eneo tulilokuwepo. Akaanza kuwapigia makofi mashabiki kwa karibu zaidi.
Mashabiki waliofurika eneo hilo wakapiga makofi kwa nguvu na baadhi yao wakaanza kutoa machozi ya furaha. Kati yao walikuwepo wasichana warembo sana.
Ndiyo, tangu natoka Tanzania nilijua kuwa Muntari ni staa sana, lakini sikujua kama alikuwa staa sana katika kiasi hicho. Zaidi ya msisimko wa mechi nilitaka kujua ni kwa nini walikuwa wameguswa sana na wachezaji wa Ghana, hasa Muntari na Michael Essien.
Shabiki mmoja aliyekaa kando yangu akaniambia ni vigumu kuwaona Muntari, Essien, Steven Appiah na wachezaji wote wa timu ya taifa ya Ghana pindi wanaporudi nyumbani kwa ajili ya likizo.
Hawa ni zaidi ya mastaa wa kawaida wa soka. Hawa ni mamilionea. Essien akirudi Ghana hapewi ulinzi kwa sababu tu ni staa, hapana ni kwa sababu pia ana fedha nyingi. Ni vigumu kumuona.
Wote wanaendesha magari ya kifahari, ambayo vioo vyao vimezibwa na rangi nyeusi. Hoteli zao huwezi kuingia. Ukionyeshwa nyumba zao utashangaa mno. Nilionyeshwa nyumba ya kiungo Layrea Kingston nilishangaa mno. Haina tofauti yoyote na ile ya mdhamini wa Yanga bwana Yusuf Manji.
Karibu watoto wote wa Ghana wanataka kucheza soka ili waishi kama wao. Hatimaye niliamini kuwa kuona ni kuamini.
Nimejikumbusha zaidi kauli hii baada ya kuona kuwa huenda bado ziara za akina Didier Drogba hapa Tanzania hazitusaidii kwa sababu kuna vitu hatuvioni kutoka kwao.
Wanapokuja wanacheza mechi flani laini laini halafu wanaondoka. Hapa ndipo akina Abduhalim Humud wanasema ‘Jamaa si lolote si chochote’. Ni vigumu kwa wachezaji wetu kubadilika kama wanaamini kuwa wanalingana na Drogba.
Lakini pia natamani hawa akina Drogba wangekuwa wanakuja na mali zao zote ndipo tungeamini kuwa jamaa ni mastaa kwa kiasi gani.
Kwa sababu hilo haliwezekani basi namuomba Mungu atupe staa wa kweli wa soka ili tujue jinsi gani akina Drogba wanaishi huko makwao.
Mungu akitupa staa wa soka watoto wote wa Tanzania watatamani kucheza Ulaya. Staa huyu kama atakuwa analipwa kiasi cha sh. milioni 250 kwa wiki basi ni wazi atatutia adabu kutokana na maisha atakayokuwa anaishi.
Mchezaji wa namna hii huwezi kumuona mtaani kirahisi. Si kwa sababu atakuwa anaringa, hapana, kwa sababu maisha yake hayatakuwa salama sana akiingia mtaa wa Tandamti pale Kariakoo.
Mchezaji huyu atakuwa anatazamwa zaidi kwa hiyo hawezi kuonekana hadharani ovyo ovyo. Ni kama ilivyo kwa mcheza kikapu Hasheem Thabeet akija Dar es Salaam siku hizi. Huwezi kumuona kirahisi.
Wapo wanaoamini kuwa labda serikali yetu iliongeza ulinzi usio wa lazima kwa akina Drogba kwa sababu ya ushamba wetu. Hapana, hata kwao hawa jamaa huwa wanalindwa hivi hivi.
Mungu akitupa staa mmoja tu nadhani wachezaji wetu wote watabadilika. Wataanza kuviona vitu kwa macho na kuanzia hapo wataamini kama mimi nilivyoamini ustaa wa Muntari pale Accra.
Lakini wakija katika ziara za kisoka hapa nchini ni vigumu kuamini kama Abdulhalim alivyoshindwa kuamini. Labda angemuona mchezaji wa Kitanzania anachezea Chelsea angeamini kuwa ni staa kiasi gani.
Ndiyo, angemuona mwenzake akikaa mtaa mmoja na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, angemuona mwenzake anaendesha gari aina ya Hammer, angemuona mwenzake akilimiliki eneo zima la Tegeta, angemuona mwenzake akimiliki nusu ya hisa za kampuni ya Vodacom. Labda angeamini.
Lakini kwa hali ilivyo sasa ni vigumu kwa mchezaji kama yeye na wachezaji wa Kitanzania kuamini. Tunaishi katika nchi ya giza, ambayo watazamaji wa soka wana uwezo mkubwa wa kifedha kuliko wachezaji.
Laiti kama tungekuwa tunaishi katika nchi ambayo wachezaji au mchezaji mmoja ni tajiri kuliko watu wote walioingia uwanjani labda tungepata adabu.
Kwa sasa naona bado hatuna adabu hata kidogo. Wachezaji wetu si mastaa na hatuna la kujifunza kutoka kwao.
Miaka kadhaa iliyopita niliitazama picha moja gazetini kwa husuda kubwa. Picha ilimuonyesha mrembo mmoja wa Kiargentina akilia baada ya kupigwa busu shavuni na nyota wa zamani wa timu ya taifa ya nchi hiyo Hernan Crespo katika uwanja wa mazoezi wa timu hiyo.
Alionekana amepagawa na alishindwa kuyazuia machozi ya furaha. Ni mrembo gani hapa nchini anaweza kupigwa busu shavuni na Mrisho Ngassa akajikuta analia kwa furaha? Hakuna.
Wachezaji wetu amkeni. Atokee walau mchezaji mmoja tu wa kuwaonyesha wengine maana ya ustaa wa ndani na nje ya uwanja. Amewaonyesha wengine maana ya soka, ustaa na utajiri.
Mimi nimeona, lakini wafanyeni wengine waone…kuona ni kuamini.