WIKI kadhaa zilizopita nilitembelewa na watu wawili wenye mipango ya kuoana, ambao kwa bahati mbaya wamejikuta wako kwenye mgogoro mkubwa na wana wasiwasi huenda wasioane.
“Uchumba wetu umeingiwa na matatizo, lililo kubwa ni kuwa mwenzangu ameporomoka kiimani; zamani alikuwa anampenda sana Mungu, siku hizi hata kusali kabla ya kula hadi nimkumbushe,mbaya zaidi ananishawishi tufanye ngono kabla ya ndoa, kitu ambacho awali tulikubaliana tusikifanye hadi baada ya kuoana,” anasema kijana aliyeongozana na msichana ambaye wanataka kuoana.
Akaongeza kuwa “Nahisi ana njia nyingine anazitegemea hasa nguvu za giza (ushirikina), ndio maana hasali kama zamani”.
“Kitu kingine kinachonikwaza sana siku moja nililala naye usiku, akawa anafanya vitu vya ajabu kama vile kuamka na hata kwenda kufungua mlango, ninapomuuliza baada ya kuamka hujibu kuwa anafanya hayo akiwa hajui. Najiuliza aaah kama kweli hajui, mbona ninapomwambia tusali hazingatii”.
Wakati mwingine pia huwa anapiga mateke na hata kusema hovyo akiwa usingizini. Kwa kweli nimekuwa na hofu naye ninaona njia sahihi ni kuachana naye, ingawa tabia hii imekuwa ikikithiri kadri miaka inavyokwenda mbele, kwani uhusiano wetu una zaidi ya miaka miwili sasa,” anasema na kuongeza kuwa anafikiri jambo la msingi kwake ili awe na amani ni kuachana naye.
Mbaya zaidi kuna siku nahisi alikuwa akinifanyia vitu vya kishirikina waziwazi… na kuanzia hapo japo nampenda sana, nikawa najilazimisha nisimpende, naumia sana ndio maana natafuta ushauri,” anasema.
Ndugu zangu ni kwamba baada ya kuwasiliana na watu hawa nililazimika kwenda kwa viongozi mbalimbali wa dini, kujadiliana nao. Aidha niliwasiliana na baadhi ya washauri wa nje ya nchi ili kwamba nitakachokiandika hapa kweli kiwe ni kile ambacho hata wengine wakikisoma waweze kukielewa vizuri.
Nafahamu safu hii imejizolea umaarufu mkubwa na kuna Watanzania wengi, maisha yao ya kila siku wanategemea ushauri huu, nimekuwa nikipokea shuhuda kutoka kwa watu wengi kwamba ndoa yangu imepona baada ya kusoma safu hii nk.
Hii ina maana kuwa ninapoombwa ushauri au ninapoandika jambo gazetini, ni lazima uwe na uhakika nalo kwa asilimia mia na kama labda kitu fulani kinaonekana kwangu ni kizito, nawasiliana na watu wengine, ili tusaidiane. Kimsingi hakuna aliyekamilika, wewe waweza kujua hili, mwenzako anajua lile, mkichanganya mnapata kitu kimoja kilicho kizuri zaidi.
ZINGATIA: Jambo la kwanza ambalo unapaswa kulifahamu ni kuwa kuzaliwa ukiwa na afya mbaya au nzuri haina maana kwamba wewe utakuwa ni mwenye afya mbaya au nzuri tu milele.
Ni kwamba kuwa kwenye uchumba wenye migogoro au amani tu, haina maana wewe utakuwa ni mwenye hali hiyo tu maisha yenu yote. Tafiti zinaonyesha kuwa wengi wa watu ambao uchumba wao umejaa amani, ndio wanaoishia kwenye majuto.
Uchumba wowote ambao watu hawajaingia kwenye migogoro, hauna maana wakioana wataishi kwa amani tu, bali ukitokea mgogoro ni vigumu watu hawa kutoachana, tofauti na wale ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa na migogoro ya hapa na pale.
Lakini jingine la kushangaza ni kwamba asilimia kubwa ya wachumba ambao wana migogoro, huwa hawaachani. Wanaweza kutengana hata kama ni miezi kadhaa, lakini hatimaye watarudiana, hasa kama watu hawa katika kugombana kwao hawafanyiani mabaya yenye kuathiri maendeleo yao ya kibiashara au uchumi kwa ujumla.
Watu wanapogombana wakati mwingine ni dalili za kupendana kupita kiasi unaosababisha wivu, hii ndio sababu ni kwanini walio wengi utaona hata kama anapigwa na kutolewa damu, bado wanaendelea kupendana, huenda ni namna ambavyo wanafanyiana mambo.
Kimsingi unapaswa kuwa makini sana unapowashauri wapenzi. Acha kusema “achana naye, kama amekufanyia hivi na vile, aaah huyo tena hakufai”….Itakuja siku utaumbuka pale watakapopendana na wewe kuonekana kwamba uliwahi kushauri waachane.
HATA KAMA HASALI SIO TATIZO: Maisha yetu yamejawa na matatizo ya hapa na pale, inapotokea mtu unamwambia kitu kizuri hafanyi, wakati zamani alikuwa anafanya unapaswa usiwe na hasira naye. Tafuta muda mzuri hasa wa kwenda naye sehemu zilizotulia kama ufukweni nk, zungumza naye vizuri, atakueleza siri zote na kwa hakika utajua ukweli.
Kuna baadhi ya watu katika mazingira yao ya kazi wamejikuta wameingizwa kwenye mikataba fulani wakati mwingine bila kufahamu kama inaweza kuwa na athari kiasi kile.
Kwa mfano kulikuwa na jamaa mmoja katika nchi fulani, yeye alikuwa kwenye kazi fulani ya ulinzi, ambayo mojawapo ya masharti ilikuwa ni kulishwa kitu fulani kama mkataba (wengine huitwa yamini) kwa ajili ya kuhakikisha anailinda nchi hasa kwa sababu alipewa kitengo muhimu sana.
Ni kwamba kama angeenda kinyume angeathirika, kwa bahati mbaya kitu kile kilimuathiri baadaye akawa analala kwa shida hadi alipokwenda kutoa taarifa na kuondolewa kwenye mfumo ule wa kazi ambayo alikuwa amepangiwa kwamba angekuwa anaifanya.
Ninachotaka kusisitiza hapa ni kwamba mwenzi wako unapoona anaonekana ni wa tofauti kaa naye chini, zungumza naye taratibu, acha kumtangaza kwa watu vibaya, wengine kazi wanazofanya wakati mwingine wanaingizwa kwenye mambo hata wasiyotaka. Unapaswa kumhakikishia kwamba siri itaendelea kuwepo hata kama atakuambia ukweli juu ya kwanini amefanya kitu fulani hata akawa hivi na vile.
Dini ni suala zito, ndio maana kuna viongozi anaweza kusema mimi wa dini fulani, lakini nyumbani kwake pia ana sehemu ya kuabudia mizimu nk, si ndio jamani? Kuna siri nyingi na nzito maisha ya watu, ili kupata ukweli kuhusu hayo, kaa na mwenzi wako aone yuko katika mikono salama, atakueleza siri zote.
NAACHANA NAYE MUNGU ATANIPA MWINGINE ANAYEFAA:Wengi wamekuwa wakijipa imani hiyo kwamba kwa sababu mwenzi wake wa sasa ana matatizo haya na yale, njia iliyo nzuri ni kuachana naye na kuwa na mwingine ambaye Mungu atampa.
Ni imani nzuri maana inasaidia pamoja na mambo mengine kuondoa msongo wa mawazo kwa baadhi ya watu…ni kama imani kwamba Yesu atarudi…toka mababu zetu hadi leo watu tunaamini atakuja…tuendelee tu kuamini kwa wale ambao tunaamini, iko siku atakuja kweli, si ndio jamani?
Ila katika maisha unapaswa kuhakikisha mchumba uliyenaye unamtengeneza hadi awe mzuri, hasa kama unayaona mapungufu yake hayaathiri sana.
Msingi wa kuishi na mtu ni kuhakikisha unazungumza naye…je kwa namna anavyoonekana ni kweli humpendi? Kama unampenda, fanya jitihada za kuwa naye…hata kama unahisi ana mwingine, jiulize kwanini awe na mwingine badala ya wewe….fanya jitihada uwe mshindi.
Siku zote katika maisha yako hakikisha wewe ndio unapendwa, na kama inatokea mwenzi wako anampenda mwingine zaidi yako, pata muda wa kutafakari ni kwanini imekuwa hivyo? Wapi umekosea hadi imetokea akafikiria kwenda kwa wengine badala ya kulipenda penzi lako?
Kimsingi si vizuri sana na wala si jambo la kufurahia kuoa unaachana na mchumba wako kwa sababu nyingi, moja ni kwamba ni kweli nafsi yako itaumia kwamba aaah nimeachana naye, pia jamii haiwezi kukuelewa leo uko na huyu kesho yule…haijengi picha nzuri.
JENGA UHUSIANO MZURI NA ULIYENAYE: Kitaalam badala ya kutafakari kwamba aaah mchumba wangu ana kasoro kwa hiyo niachane naye, tafakari namna ya kuimarisha uhusiano wenu. Unachonena ndicho kitakachotokea, nena juu ya namna ya kufanya ili uwe na ndoa nzuri, hakika utafanikiwa hilo, ukinena kuachana kweli nalo linaweza kutokea.
Kama ambavyo mkulima shambani kwake kukiota majani, anatafuta dawa ya kuua majani, nawe unapokuwa na tatizo, tafakari kwa makini namna ya kupata dawa. Lakini zaidi ya yote tafakari pia juu ya mtu huyo, je hata ndugu zake wanamzungumziaje? Kama wanamzungumzia vizuri, ni wazi unapaswa kuendelea naye, lakini kama wanamzungumzia vibaya, tafakari kwa makini, ikiwezekana achana naye kabisa.
Tafakari juu ya kuendelea na mtu ambaye nafsi yako kweli inamuwaza hata kama mmeachana, huenda ni kwa matendo yake mazuri, huenda ni siku zile za upendo mzuri nk, huenda ni msaada wake katika maisha yake nk, sahau mabaya yake, mpe muda kurekebisha kasoro zake.
Hata kama unahisi si mwaminifu, jiulize ni wapi hasa ameanza kuonyesha hiyo kasoro? Wengine wanaweza kutokuwa waaminifu labda ni kwa sababu tu anaona mwelekeo wa uhusiano umekuwa mbaya nk.
MSISITIZO:Msingi wa kuwa na ndoa nzuri ni wewe mwenyewe, usiwe na hasira, mpe muda mwenzi wako kuzungumza naye, kwa hakika nakwambia atakueleza hadi siri ambazo hujawahi kuambiwa. Cha msingi uwe mpole, wala usiwe na haraka katika kujua kile ambacho una shauku nacho. Haraka-haraka haina baraka.
NI KWANINI WATU WANAOANA?: Ukiwauliza watu wengi ni kwanini mnaoana watakwambia ni kwa sababu wanasaka upendo, furaha, amani na ridhiko kutoka kwa yule anayeoana naye.
Wengine wanakwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa Mungu anataka watu waoane ili wakaijaze nchi…mhh dini iko kwenye hili tu, vipi maisha yenu mengine kama ni kweli tunapenda kufuata ya Mungu?
UKWELI UKOJE? Tafiti nyingi duniani zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia70 ya ndoa hazina amani ambayo watu walikuwa wakiitarajia. Ndoa imekuwa ni kama kamba au mnyonyoro wa kuwafunga na kuwavutia watu kwenye matatizo.
Ndoa imekuwa ni sehemu ya matatizo, badala ya faraja. Iwe umeoana na mtu wa namna gani, bado wakati mwingine hutokea mikwaruzo ya hapa na pale. Kama unafikiria ndoa ni amani tu milele, ndoa haikufai. Badala yake unapaswa kufahamu kuwa ndoa kama yalivyo maisha ya aina nyingine, suala la kukwaruzana ni la kawaida, cha msingi ni kufahamu namna ya kuondoa kasoro ili muweze kuishi kwa amani.
Msingi wa kuwa na ndoa yenye amani ni kwa wahusika kwanza kusomana tabia kwamba huyu anataka nini au hataki nini, kisha kufanya yale ambayo yanaonekana ni yenye maana kwa mwingine.
Je mwenzi wako anaweza kubadilika kitabia? Hili ni suala jingine la msingi. Ikiwa mwenzi wako anaonekana mwenye tabia mbaya, angalia kama anaweza kubadilika, je ni mtu ambaye mnaweza kuzungumza na akawa mwenye tabia nzuri? Je anaonekana kukubembeleza kwa dhati ili mrudiane?
Ukitaka kujua kama kweli fulani anakupenda au la, pamoja na mambo mengine ni namna ambavyo anakusumbua baada ya kuwa tayari mmeachana, yawezekana ni kwa njia ya ujumbe kwenye simu yako au kuwasiliana na watu wa karibu naye.
Mtu wa aina hii ni vizuri kumfikiria kurudiana naye kwa sababu ni wazi atakuwa anaumia moyo wake, atakuwa anafanya lile awezalo kuhakikisha hamuachani tena.
Hata kama analinga kwa kiasi gani, je inapofikia hatua kwamba unamwambia kuanzia leo tuachane nafsi yake inakuwaje? Anakusumbua au anaona ni sawa tu? Angalia hili kwa umakini. Ukweli ni kuwa licha ya wengine kuwa jeuli, anapoona kweli mnaachana huwa wanaumia na hapo ndipo huwa wanaanza kuchukua hatua za kutaka kurudiana na pia kuanza kuchukua hatua za kurekebisha kasoro zote.
KWANINI NDOA NI NGUMU? Kuna taarifa nyingi zinaonyesha kuwa ndoa zimejaa matatizo. Msingi wa hali hii ni wanandoa wenyewe, walio wengi kutopeana nafasi ya kurekebishana kasoro ambazo mmoja ameziona kwa mwingine.
Hata kama mwenzi wako ni mbaya kwa mfano unaamini amewahi kujiingiza kwenye vitu vya ajabu, ndugu yangu mhhh watu hubadilika tabia…alikuwa mchawi, leo unasikia ameokoka, si ndio jamani? Ndoa inakuwa ngumu pale mmoja anapolazimisha mwingine abadilike tabia au aache kitu fulani kwa muda mfupi…bila kutafakari kwa makini kwanini leo amekuwa hivi wakati jana alikuwa vile.
Ndoa ni ngumu na nini kifanyike ili zisiwe ngumu, ziwe nzuri, tamu na nyepesi? Kuna watu waliachana na wachumba wakiamini watapata walio wazuri…wakajikuta wamepata wabaya zaidi na walioawaacha.
Swali hapa ni je unachana na mchumba fulani ukiamini utapata mzuri, nini kinakupa matumaini hayo? Kwanini usifanye jitihada kuelewana vizuri na uliyenaye badala ya kuruka-ruka, mara leo huyu kesho yule?
VISA NA MIGORORO DAWA YAKE IPO; Katika baadhi ya mahusiano watu utakuta wanawekeana visa hasa baada ya kutokea migogoro. Ukifuatilia vile visa na vikwazo katika ndoa, utagundua kwamba huletwa zaidi na kufikiri kwetu kubaya, kutazama pabaya zaidi badala ya pazuri. Kuna watu utaona anachokiwaza zaidi juu ya mwingine ni namna ya kufanya ubaya, badala ya mazuri kitu ambacho si sahihi katika maisha.
Kufikiri huku huanzia mbali, huanza tukiwa wadogo, wakati wa uchumba na mara nyingine siku ya ndoa yenyewe. Tukiwa wadogo huwa tunaonywa juu ya uwezekano wa kupata wenza wabaya au kuwafanyia ubaya kama vile kuwapiga, kuwasaliti nakadhalika.
Hali kadhalika wengine wamekuwa ni wazuri wa kupokea ushauri wenye kuambatana na maonyo juu ya uwezekano wetu wa kuwapiga au kupigwa na wenza wetu.
Hata katika siku za harusi, ujumbe mkuwa huwa ni maneno kama usimpige, na mwanamke huambiwa asimzadharau, neno msamaha huwa halizingatiwi sana. Hata mikanda mingi ya televisheni inayozungumzia ndoa ni ile inayoeleza zaidi kuhusu haya ya mke kumheshimu mume, mke asimdharau mume nk.
Katika ndoa nyingi watu tunayapa kipaumbele matatizo ya wenzetu na kuyapa kipaumbele na kuanza kuona kama hawafai na hawana msaada wowote kwetu na kwa hiyo tunapaswa kuwatendea ubaya.
Aidha baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yenye kuwasaidia wanawake, wanachowashauri zaidi wanawake ni kwamba kama wameolewa na wanaume wakorofi, waachane nao, badala ya kuwasaidia kubadilika ingawa kwa baadhi ya wanaume hasa wenye umri wa zaidi ya miaka 35 huwa ni vigumu kubadilika tabia hata ufanyeje.
MSINGI MZURI WA MAISHA:Tunapofikiri wenza wetu wana ubaya, basi suruhu ni kushirikiana nao ili kuushinda huo ubaya, badala ya kuwaza namna ya kuachana nao. Kama kwa mfano mchumba wako ni mbaya labda anaendekeza ngono nk, unachotakiwa kufanya ni kumsaidia kuondoa kasoro hiyo ambayo kimsingi inaweza kuondoka, ili mradi tu kama mtu mwenyewe atapatiwa kile ambacho anakihitaji.
Tusipofanya jitihada za kuwapenda wenye kasoro, basi na sisi tunakuwa sehemu ya huo ubaya na kuukuza na wakati mwingine sisi ndio chanzo cha huo ubaya tunaouona kwa wengine.
Kumbuka uchumba au ndoa ni lazima iwe na changamoto na dawa ya changamoto ni kuzipokea na kuzikubali ili kuzikabili salama. Vinginevyo ni kushindwa na kuishia kubaya. Sisi ndio msingi ya mafanikio ya ndoa zetu. Furaha, amani na ridhiko katika ndoa zetu, vimo ndani mwetu na sio nje yetu. Je wewe unafanya nini ili kuhakikisha unakuwa na amani ya dhati katika uhusianio ulioko?
Ikiwa mtu wako unapokuwa naye unapata raha ya dhati yawezekana ni katika tendo la ndoa, anakupa amani kwa maana pia ya kiuchumi kwamba anakusaidia kimawazo na wala haonyeshi kuhangaika na mali zako nk, huyo ni aina ya mtu ambaye kumfikiria kama ni mtu mwenye kukufaa, ndio kusema kuwa angalia namna ya kufanya ili uweze kuwa na amani ya dhatio naye.
Dismas Lyassa ni mtaalam wa mahusiano aliyesajiliwa na serikali (Social Welfare Counselor), wasiliana naye 0754 498972