KARIBUNI katika siku nyingine nzuri ya Jumanne hasa katika safu hii ambayo imekuwa ni msaada mkubwa katika kuimarisha uchumba na ndoa.
Niwakumbushe tu wapenzi wasomaji kuwa nimepanga vizuri kuhakikisha katika safu hii vitu vinaandikwa kitaalam zaidi na vina maana kwa msomaji, najiandaa kusoma zaidi kwa njia ya posta katika chuo kiitwacho The Kinsey Institute for Research in Sex, Gender, and Reproduction, Inc, kilichoko India na Marekani.
Kozi nitakayosomea itahusisha namna gani wanandoa wanapaswa kufurahiana, nikiwa na imani kuwa itanisaidia kuwa bora zaidi kwenu katika kuandika na maisha yangu kwa ujumla kwani elimu kwa hakika haina mwisho.
Endeleeni kusoma safu hii na zaidi ya yote wakumbushe na wengine kuisoma, nina imani itaendelea kuwa msaada zaidi.
Kitaalam unapaswa kusoma zaidi kazi za watu ili kuongeza ujuzi kutoka kwenye ule ambao unao. Ndio maana huwa nawaasa watu katika maisha kupenda kufuatilia mambo ya wenzao hasa wale ambao wanaendesha mambo yao vizuri, ili nao waige mazuri hayo.
NI MUHIMU ZAIDI KUFAHAMU: Unapofikiria kuingia kwenye ndoa, fahamu kuwa ni sehemu ya kwanza muhimu, na kwamba bado sehemu nyingine ambayo ndio muhimu zaidi.
Ni kuwa kuingia kwenye ndoa ni jambo muhimu, lakini lililo muhimu zaidi ni kujua nini cha kufanya ili uwe na maisha bora zaidi yenye amani.
Wakati fulani niliwahi kukutana na kijana mmoja alilalamikia kuwa hafahamu ni namna gani anaweza kufanya ili kushirikiana na mpenzi wake.
"Sijui namna gani nifanye maana sifahamu namna ya kushirikiana na mpenzi wangu, mara nyingi anasema simfurahishi," anasema kijana huyo.
Kitaalam ni ukweli kwamba kuwa Mwanaume au Mwanamke haina maana kwamba tayari wewe ni MKE au MUME. Kuna sifa ambazo mtu anapaswa kuwa nazo ndio awe MKE au MUME, mojawapo ni kujua kile ambacho kinakupasa kufanya.
Kuwa na mwili mkubwa sio maana yake utakuwa bondia mzuri, si ndio jamani? Haya mambo tuyatafakari kwa umakini, maana wapo watu wanaamini kuwa kwa sababu ana mwili basi tayari yeye ni mzuri au anaweza kufanya kitu fulani.
Kuna mwanaume mmoja juzi alinipigia simu akisema ‘Dismas ndugu yangu mapenzi hayana sababu ya kusomea, ni suala la kufanya tu basi”…Ni wengi wanaamini hivyo, kitu ambacho si kweli.
Tangu zamani watu walikuwa wakisomea, japo si elimu ya muda mrefu, nafikiri utakubaliana nami kuwa katika mila nyingi za Tanzania kulikuwa na jando la unyago, kwamba binti huyu kijana alikuwa akienda kufundishwa namna gani anapaswa kuishi na mke au mumewe.
Walikuwa wakifundishwa mambo mengi, hata miondoko, eeeh kwamba mwenzi wako akiwa mja mzito kwa mfano ‘ondoka’ naye katika muondoko wa aina fulani…kwa sababu ya kutokuwa na elimu ya kutosha, baadhi ya wanaume wamejikuta wanaharibu mimba za wake zao. Kisa ameondoka muondoko usifaa.
Lakini ipo shida kwa baadhi ya watu, kwamba uko naye, mko faragha na mwandani wako. Ukajitahidi kuhakikisha unateka hisia zake ipasavyo na kumfanya afurahie kuwa na wewe, kumbe unajisumbua!
Tatizo hili ni gumu kidogo kuonekana moja kwa moja, kwani wengi huwa wanaogopa kusema ukweli, lakini ni tatizo sugu maana hadi ugundue kwamba humridhishi mpenzi wako huwa hali imeshakuwa mbaya na wakati mwingine inaweza kuwa mwisho wa penzi lenu.
Ili usipatwe na matatizo hayo, ni vyema kama utaishughulisha akili yako zaidi, wewe mwenyewe uhakikishe unafanya kila kilicho kizuri ili kumfurahisha badala ya kumboa mwandani wako. Kuboa ninakosema ni pamoja na kufanya kitu ambacho tayari mwenzi wako ameshakuambia kuwa hakitaki.
UHURU NI MUHIMU; Mnapokuwa na mwenzi wako anapaswa kuwa huru kwa chochote anachotaka. Mnapoona mwili wako ni mali yake na mwili wake ni mali yako.
Ikiwa hutakuwa makini na haya nikuambiayo, usishangae siku moja unaletewa nyumba ndogo na mumeo, zuia hilo kwa kuwa karibu na mpenzi wako, fahamu wezi wa ndoa siku zote wanajua mbinu nyingi za kumpagawisha mpenzi wako akuone huna lolote na pengine kujikuta amehama nyumbani au kukuona kero ndani ya nyumba yenu.
Je, wewe unayesoma makala hii uhusiano wako ukoje? Kimsingi unapaswa kuangalia ni wapi umekosea. Wakati fulani nilikutana na mwanaume mmoja akilalamikia mkewe kwenda nje…swali la kujiuliza hapa ni kwanini aende kwa wengine na kukuacha wewe?
Kitaalam watu husaka furaha, na mbaya zaidi kuna baadhi ya watu kwa sababu labda amekuwa akifanya tendo la ndoa kwa miaka mingi, inapotokea kukatokea hali ya kutoelewana, baadhi yao huwa kama ni wenye kuwehuka kwa kusaka wanawake ovyo. Siri ya kuishi na mwanaume wa aina hii ni kuzungumza naye, kwani ni tatizo linalowasumbua wanaume wengi.
Kimsingi mpe uhuru mpenzi wako ili aweze kulifurahia penzi lako, hapo sasa ndipo fikra za kutafuta kimwana nje zitakapofutika akilini mwake.
Dismas Lyassa ni mtaalam wa uhusiano aliyesajiliwa na serikali kutoa ushauri (Social Welfare Counselor) 0754 498972