JAJI wa Beverly Hills, Marsha Revel amefuta kibali cha kumkamata muigizaji Lindsay Lohan baada ya wakili wa muigizaji huyo kuonyesha vielelezo vilivyothibitisha kwamba dada huyo amekuwa akihudhuria darasa maalum la ushauri wa kuacha pombe.
Lindsay aliwahi kufikishwa mahakamani mwaka 2007 kwa kosa la kutumia kiasi kikubwa cha kilevi na alitakiwa kuanza kuhudhuria darasa la ushauri maalum wa kupunguza utumiaji wa pombe.
Lakini baadaye kulikuwa na taarifa kwamba Lindsay hakuwa akihudhuria darasa hilo.
"Pamoja na kwamba kulikuwa na malalamiko hayo, lakini wakili wa Lohan alifikisha vithibitisho mahakamani vinavyoonyesha kwamba mwanamke huyo amekuwa akihudhuria darasa na hakukuwa na matatizo yoyote," ilisema taarifa ya polisi.
Ingawa kuna habari kwamba nyota huyo wa filamu amedaiwa kuhudhuria darasa hilo lakini waandishi wa habari wameshikwa na mshangao kwa sababu hakuna hata siku moja, ambayo walifanikiwa kumuona Lindsay eneo la ushauri licha ya kumuwinda kila mara.