Takukuru imulike uchaguzi mkuu wa TFF

MCHAKATO wa uchaguzi ndani ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) unaendelea, lakini kumekuwa na wito kutoka kila pande kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) isikae mbali na uchaguzi huo.

Karibu kila mdau wa soka anayehojiwa wakiwamo waliowahi kushika nyadhifa kubwa kwenye soka la Tanzania, wanatoa wito kwa Takukuru kutupia jicho uchaguzi huo kwa madai kwamba huenda rushwa ikatumika kushawishi wapiga kura.

Kwa kuzingatia usemi wa wahenga kwamba ‘lisemwalo lipo na kama halipo basi linakuja’, si wakati wa Takukuru kupuuza wito huo. Kauli hizi za wadau hazipaswi kuchukuliwa kama mzaha na badala yake zifanyiwe kazi kwa weledi wa hali ya juu ili kiongozi atakayechaguliwa apatikane kwa haki.

Hali  ya hofu inakuwa kubwa zaidi pale mmoja wa makatibu wakuu wa zamani wa TFF alipoweka hadharani kwamba ipo haja ya Takukuru kukaa macho wazi kwani mambo yanaweza kupindishwa kwa asante ya rushwa.

Inapofikia hatua mtu ambaye amekuwepo kwenye mpira kwa miaka zaidi ya 20 anatoa kauli kama hiyo, si jambo la kupuuza hata kidogo. Takukuru inapaswa kujiweka karibu na uchaguzi huo ili kuzuia mianya yote ya rushwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wapige kura kwa haki.

Siku zote imekuwa ni rahisi kwa chaguzi kama hizi zinazohusisha wapiga kura wachache kugubikwa na rushwa kwani ni rahisi kuwafikia wapiga kura hao na kuwapatia chochote kitu.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF ambao ndio wapiga kura, hawazidi 150 hivyo ni rahisi kwa mgombea yeyote kuwashawishi kwa fedha ama zawadi nyingine ili waweze kumchagua na ndiyo sababu Takukuru imeombwa kusogea karibu.

Tunashukuru kuona baadhi ya viongozi wa Takukuru wakikiri kuwa tayari wamepachika watu wao katika uchaguzi huo ili kuona kila kitu kinakwenda kama ilivyotakiwa, lakini tungependa kuwapa wito wa kuongeza nguvu zaidi.

Taa ya kumulika kama kuna viashiria vya rushwa isiwepo tu jijini Dar es Salaam kama ilivyozoeleka, bali iwepo katika maeneo mengi zaidi ambayo yanagusa uchaguzi huo.

Yawezekana wapo baadhi ya wapiga kura ambao tayari wamejiandaa kurubuniwa ili kupata chochote kitu kwani wamekuwa wakitumia nafasi zao kama mitaji badala ya kuamua hatma ya soka la Tanzania ambalo kwa sasa limepoteza mwelekeo kwa kiasi kikubwa.

Imefikia hatua sasa hata wagombea wa nafasi hizo wamekuwa wakipigana vikumbo na kuchuana vikali, siyo kwa sababu wanaupenda sana mpira wa Tanzania, bali kwa kuwa wameona kwenye soka ni sehemu ambayo ina pesa zinazoweza kuchukuliwa kirahisi.

Tukumbuke kuwa chaguzi kama hizi mara nyingi zimekuwa zikivurugwa na wenye kitu mkononi, jambo ambalo linapunguza msisimko wa soka la Tanzania.

Imefika pahala sasa kama Tanzania tusimame pamoja na kusema hapana kwa wale ambao wanapenda kuingia kwenye soka kwa kupitia mlango wa nyuma hasa kwa kuwarubuni wapiga kura.

Tunapenda kutoa rai pia kwa wajumbe ambao watahusika kupiga kura, wachukue hatua pia kuwaripoti wagombea wote ambao wanajihusisha na vitendo vya rushwa.

Tumeona Serikali ya Awamu ya Tano ilivyo makini katika kuhakikisha rushwa inapungua, hivyo tusimame imara kuhakikisha kwamba tunakuwa msaada kwao.

Mwisho wa yote tuiombe Takukuru kushirikiana kwa karibu na wadau wote muhimu ili kusimamia uchaguzi huo na kuhakikisha kwamba rushwa haipewi kipaumbele kabisa ili tuwapate viongozi safi wa kuongoza soka la Tanzania.