Zahera wiki tu inamtosha Yanga

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, ameweka wazi kuwa anahitaji siku nane tu kuanzia sasa ili kukamilisha jeshi lake la msimu ujao na ndipo ataanza rasmi maandalizi ya mechi zijazo za kimataifa.

Nyota wa Yanga sasa wapo mapumzikoni huku viongozi wa klabu hiyo wakiendelea na usajili ambao unazingatia maelekezo ya kocha huyo Mkongomani ambaye ameahidi kuwa timu hiyo itashusha nyota wa maana.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo alisema kwa sasa yupo mapumziko na hawezi kuweka wazi ni hatua gani ya usajili imefikiwa na uongozi ambao tayari aliukabidhi majina ya nyota anaowahitaji.

Zahera alisema mpaka Juni 25 usajili utakuwa umekamilika kwa kiasi kikubwa ambapo ataanza rasmi maandalizi ya kuivaa Gor Mahia katika mechi ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

“Nimeikuta Yanga ikiwa inaelekea kumaliza msimu, nilikua siwajui vizuri wachezaji, lakini nimeweza kukaa pamoja na kocha msaidizi niliyemkuta kwa ajili ya kuandaa ripoti ambayo niliwaachia viongozi, naamini wameifanyia kazi kwani niliwaambia hadi ifikapo tarehe 25 wawe wamekamilisha,” alisema.

Zahera alisema wachezaji wengi walitaka kujiunga na timu kabla ya mapumziko ya sasa, lakini aliwazuia kwasababu alihofia watatumia gharama kubwa kulala mahotelini wakati bado timu haijaanza maandalizi ya msimu ujao.