#WC2018:Russia 2018 bila mavitu ya Alexis Sanchez

Muktasari:

  • Kila mchezaji wa timu ya taifa pamoja na makocha wanatamani kuzisaidia timu zao kunyakua ubingwa wa fainali hizo ambazo ni kubwa kwa timu za taifa.

MOSCOW, RUSSIA
FAINALI za Kombe la Dunia 2018 nchini Russia zikiwa zinakaribia kuanza, taifa la Russia na dunia kwa ujumla inasubiria kuwaona mastaa mbalimbali wa soka wakionyesha maajabu yao uwanjani.
Kila mchezaji wa timu ya taifa pamoja na makocha wanatamani kuzisaidia timu zao kunyakua ubingwa wa fainali hizo ambazo ni kubwa kwa timu za taifa.
Baada ya safari ndefu ya mechi za kufuzu, safari ambayo ilishuhudia vicheko na vilio kwa baadhi ya mataifa na hatimae mataifa 32 yalipatikana nafasi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 2018.
Baada ya mataifa makubwa kama Uholanzi, Italia na Marekani kukosa nafasi ya kufuzu, ndipo unapogundua kuwa kuna baadhi ya mastaa ambao watatazama fainali hizo wakiwa kwenye sebule za nyumba zao na itaingia katika kumbukumbu za fainali hizo za dunia.
Wafuatao ni nyota watano ambao wapenda soka hawatapa bahati ya kuwashuhudia nchini Russia katika Fainali za Kombe la Dunia 2018 kwa sababu mataifa yao yameshindwa kufuzu:


 5. Arturo Vidal (Chile)
Kipigo dhidi ya Brazil pamoja na matokeo mabaya ya mechi nyingine za kufuzu ni baadhi ya vitu vilivyochangia Chile kukosa nafasi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu.
Kokosa nafasi kwa taifa hili, kulishuhudia muunganiko wa kizazi cha dhahabu cha Chile kikiongozwa na kiungo Arturo Vidal, kutazama fainali hizo wakiwa kwenye sebule za nyumba zao.
Vidal alikuwa nguzo muhimu kwenye kikosi cha Chile kilichotwaa ubingwa wa Copa America mara mbili mfululizo na amefanikiwa kuichezea timu hiyo zaidi ya michezo 90 mpaka sasa.


4. Leonardo Bonucci (Italia)
Bonucci ni mmoja kati ya walinzi bora wa kati kwa sasa barani Ulaya. Ndoto ya Bonucci kuiwakilisha Italia ‘The Azzurri’ kwenye Fainali za Kombe la Dunia 2018 ilifutika baada ya timu hiyo kufungwa na Sweden kwenye mechi ya kwanza ya hatua ya mtoano (Play-off) na kulazimishwa sare ya 0-0 nyumbani kwenye mechi ya marudiano.


3. Alexis Sanchez (Chile)
Nguvu, kasi, uwezo wa kupiga chenga na kuwahadaa walinzi wa timu pinzani ni miongoni mwa sifa za Sanchez. Kama ilivyo kwa Vidal, kwenye Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu hatutamshuhudia mshambuliaji huyu kutokana na Chile kushindwa kufuzu.


2. Arjen Robben (Uholanzi)
Nadhani huyu ni nyota ambaye ahitaji utambulisho sana kutokana na jina alilojijengea kwenye medani ya soka kwa kipaji chake cha hali ya juu.
Baada ya Uholanzi kushindwa kufuzu Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu, wapenda soka wengi walisikitishwa kutokana na kukosekana kwa vitu vya kusisimua anavyovifanya Robben awapo uwanjani.
Akiwa na umri wa miaka 34, Robben amekuwa akikabiliwa na majeraha ya mara kwa mara, lakini akiwa kwenye kiwango chake bora unaweza ukakataa kama ana umri mkubwa.


1. Gianluigi Buffon (Italia)
Buffon ni miongoni mwa magwiji wa soka nchini Italia na duniani. Ndoto zake za kwenda Russia kuiwakilisha timu ya taifa ya Italia zilifutika baada ya timu hiyo kutolewa na Sweden kwenye mechi za mtoano (Play-offs) za kufuzu fainali hizo. Buffon ameichezea Italia ‘The Azzurri’ jumla ya michezo 176.