#WC2018:Pacha wa Messi Russia 2018 pasua kichwa

Muktasari:

  • Kocha wa Argentina, Jorge Sampaoli ana kibarua kizito cha kumtafutia Messi wanajeshi watakaomsaidia kutengeneza historia ya muda mrefu ya kunyakua ubingwa wa dunia anayoiwaza. Hebu tujongee sote kuwachambua:

BUENOS AIRES, ARGENTINA
LIONEL Messi “La Pulga” amejihakikishia namba katika  kikosi cha Argentina, lakini wasiwasi umeibuka juu ya nani atakuwa pacha wake kwenye fowadi ya timu hiyo katika fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika huko Russia baadaye mwaka huu.
Kocha wa Argentina, Jorge Sampaoli ana kibarua kizito cha kumtafutia Messi wanajeshi watakaomsaidia kutengeneza historia ya muda mrefu ya kunyakua ubingwa wa dunia anayoiwaza. Hebu tujongee sote kuwachambua:


#1 Sergio Aguero
Bila ya kupepesa macho, huyu ni chaguo sahihi la Messi katika eneo la mwisho la timu pinzani. Aguero ni kama amefufuka upya tangu kuwasili kwa meneja Pep Guardiola katika kikosi cha Manchester City na kuwa miongoni mwa wafumania nyavu bora. Mshambuliaji huyu ambaye mara kadhaa ameonekana kutokuwa katika kiwango bora katika michezo mingi ya nyumbani kwa taifa lake na kusemekana kufichwa katika mechi kubwa, huduma yake haikupatikana katika mechi za kirafiki za kimataifa zilizofanyika wiki hii kutokana na kupata majeraha. Hata hivyo, hali hiyo haikatishi matumaini yake ya kwenda Russia. Ana uhakika wa kurudi kikosini kama atakuwa fiti.


#2 Gonzalo Higuain
Mshambuliaji tegemezi wa Juventus amekuwa akitumiwa katika nafasi mbalimbali na kocha wake Jorgi Sampaoli tangu alipochukua mikoba ya Edgardo Bauza katikati ya safari mwaka 2017. Higuain amecheza mchezo mmoja tu akiwa chini ya kocha huyu, ushindi bora kabisa dhidi ya Brazil katika mchezo wa kirafiki, na aliachwa nje katika michezo ya mwisho ya kufuzu ya Kombe la Dunia. Yupo katika kiwango kizuri akiwa na klabu yake ya Juve, lakini ana nafasi bado ya kupigania namba kule Russia akiwa anajiandaa kuanza moja kwa moja katika mitanange ijayo akiwa na ndiyo chaguo la kwanza la Albiceleste kutokana na majeraha ya Aguero.
#3 Mauro Icardi
Mabao manne katika ushindi wa Inter wa mabao 5-0 dhidi ya Sampdoria wiki mbili zilizopita yalikuwa majibu mazuri kutoka kwa Icardi baada ya nyota huyu kuachwa nje katika kikosi cha Sampaoli kilichokabiliana na Hispania na Italia hivi karibuni katika mechi za kirafiki za kimataifa. Ni mfungaji thabiti wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A). Kwa miaka sasa, Icardi amekuwa akipambana kujaribu kurudisha kiwango chake katika ngazi ya kimataifa, huku akiwa bado hajafunga katika michezo minne aliyoichezea akiwa na jezi ya Argentina. Kocha alieleza Alhamisi kuwa alishtushwa kuona kikosi chake cha Argentina kikipungua makali yake, licha ya ukweli kwamba ni mapema sana kuwaondoa katika mbio hizo za ubingwa wa dunia moja kwa moja.


#4 Paulo Dybala
Sambamba na Icardi, Kiungo mchezeshaji huyu wa Juventus atatazama mechi hizi za kimataifa akiwa nyumbani kwake baada ya Sampaoli kumbwaga katika kikosi chake. Ni kweli kuwa licha ya kuwa na kipawa maridhawa, Dybala bado hajaweza kumshawishi kocha kumjumuisha kikosini. Mjadala wa namna gani anaweza kupangwa pembeni ya Messi umekuwa ukileta utata mkubwa. Vikwazo vya namna hiyo vimekuwa vikiminya nafasi ya Dybala kuelekea Kombe la Dunia, huku Sampaoli akisema bayana ndani ya wiki hii kuwa nyota huyo ameanza taratibu kupoteza nafasi ya kuchaguliwa kikosini. Licha ya hayo Icardi ataendelea kupambana mpaka nukta ya mwisho.


5 Angel Correa
Wakati majeraha yakimweka nje Aguero katika michezo ya mwezi Machi, Sampaoli aliigeukia moja ya sura ambazo hazikutegemewa na watu wengi ili aweze kuziba nafasi katika kikosi chake. Correa huyu ni roho ya Atletico Madrid na ameweza kuwapiku nyota wote wawili Icardi na Dybala kuchukua nafasi kikosini. Nafasi hiyo imepatikana huku pongezi nyingi zikiangukia kiwango chake bora sana pale Wanda Metropolitana. Mchezaji huyu (23) anakuwa sehemu ya kukiongezea upana kikosi hiko akiwa kama kiungo na pia akiwa kama mshambuliaji katika kikosi cha Argentina.


6 Lautaro Martinez
Akiwa tu na umri wa miaka 20, kinda huyu machachari wa Racing Club kwa sasa ndiyo anayezungumzwa sana.  Sampaoli ameshatembelea pale Cilindro si chini ya mara tatu kumwangalia Martinez ambaye alimkuna kocha huyo wa Argentina kwa rekodi yake ya kushangaza ya mabao 7 iliyomuhakikishia nafasi kwenye kikosi cha wakubwa. Fainali hizo za Kombe la Dunia zimekuwa ni za mapema sana kwa mshambuliaji huyu, lakini kipaji chake kilicho dhahiri pamoja na uwezo madhubuti ulionyeshwa katika mitanange kadhaa umeweka usawa na unaweza ukampatia fursa ya kupata namba Russia.


#7 Cristian Pavon
Nyota huyu wa Boca Juniors anaungana na Martinez katika kikosi hicho, likiwa ni chaguo lingine la Sampaoli kutoka katika Ligi Kuu ya Argentina. Pavot ameonyesha uwezo mkubwa sana katika mchezo wake wa kwanza wa kimataifa mwezi Novemba mwaka jana, akitengeneza mabao mawili kwa Aguero katika michezo dhidi ya Russia na Nigeria, ufundi wake unamfanya kuwa chaguo muhimu katika kikosi hicho cha Argentina kilichosheheni nyota wengi.


8 Dario Benedetto
Kama isingekuwa kupata kwa majeraha ya kifundo cha mguu mwezi Novemba, Benedetto angekuwa na nafasi ya kuingia moja kwa moja katika orodha ya wachezaji wa Argentina kwa ajili ya Kombe la Dunia. Mshambuliaji huyu wa Boca Juniors ameshawaka kimyani mabao 12 katika michezo mingi kabla ya kuwa majeruhi, pia aliweza kucheza katika michezo minne ya kufuzu ya Argentina bila ya kufunga.  Licha ya ukweli anapambana kurudi katika michezo ya kiushindani kabla ya mwezi Juni lakini ndoto ya Kombe la Dunia imeisha.