#WC2018: Ni watu wa mpira, lakini hawafuatilii Kombe la Dunia

KUTOPATA nafasi ya kuwa kwenye fainali za Kombe la Dunia, hutoa fursa kubwa ya kujipumzisha kwa baadhi ya wacheza soka na makocha pia.

Baada ya kutoka kwenye purukushani nyingi za msimu mzima, kuna wachezaji wameamua kutumia fursa ya wakati huu kujipumzisha hasa ukizingatia hawapo kwenye fainali za hizo zinazoendelea kule Russia.

Watu hawa wa mpira wamekuwa bize kufanya mambo mengine ya kujifurahisha na kusahau kabisa kama kwa sasa kuna michuano mikubwa kabisa ya mchezo wa soka, Kombe la Dunia.

5. Fabinho

Mashabiki wa Liverpool wamekosa fursa ya kumtazama staa wao mpya akikipiga huko kwenye fainali za Kombe la Dunia. Fabinho hakuitwa kwenye kikosi cha Brazil na kuona hivyo, hakutaka kujipa tabu, baada ya kukamilisha tu dili la kujiunga na Liverpool akitokea AS Monaco, Mbrazili huyo kiraka aliamua kumchukua mke wake na kwenda naye mapumziko huko Miami, Marekani. Amekwenda ‘kuchaji betri’ kabla ya msimu mpya kuanza.

4. Memphis Depay

Kuna habari zinafichua kwamba Memphis Depay amekubali kusaini dili la miaka mitano huko AC Milan. Lakini, kilichobaki ni kwamba wababe hao wa Serie A bado hawajafikia makubaliano na Lyon juu ya ada.

Baada ya kusikia kuna dili hilo, Depay, ambaye anapenda maisha ya starehe, ameamua kwenda kujipa raha na marafiki zake. Winga huyo wa Kidachi ambaye timu yake ya Uholanzi imeshindwa kufuzu fainali hizo za Russia, alionekana akiwa kwenye boti moja ya kukodi, akipozi na marafiki zake huku akipuliza tu sigara. Hayo mambo yote yanafanyika kwenye bahari ya Mediterranean.

3. Jurgen Klopp

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp, ameamua kumchukua mke wake, Ulla na kwenda naye kuponda raha huko Saint Tropez, Ufaransa.

Klopp amekwenda kujipumzisha na alionekana akipiga pombe kujaribu kujisahaulisha kile kilichotokea kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati kikosi chake cha Liverpool kilipochapwa na Real Madrid.

Klopp aliungana na marafiki zake pamoja na wanafamilia wengine na kuonekana kabisa kwamba hana haja ya kujua kinachoendelea kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia.

2. Nathan Ake

Nathan Ake alifahamika wazi kwamba kipindi hiki atakuwa kwenye mapumziko kweli kweli hasa baada ya timu yake ya taifa, Uholanzi kushindwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia huko Russia.

Baada ya kuona taifa lake limeshindwa kufuzu, Ake, ambaye ni beki wa kati, hakutaka kujihangaisha kuangalia fainali hizo na badala yake amekwenda kula zake raha na mpenzi wake.

1. Karim Benzema

Straika wa Real Madrid, Karim Benzema, amekuwa na uhusiano mbaya na timu ya taifa ya Ufaransa na mara zote amekuwa akiwekwa kando na kocha Didier Deschamps.

Lakini, kwa sasa wakati kikosi cha Les Bleus kikiwa bize huko kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Russia, Benzema ameamua kwenda zake kuponda raha, akiwa zake mapumziko Miami, Marekani.