#WC2018:Nenda kawatazame Russia 2018

MOSCOW, RUSSIA


KOMBE la Dunia bado linahesabika kuwa moja ya michuano yenye hadhi kubwa kwenye mchezo wa soka duniani na kwa kipindi hiki ambacho fainali za huko Russia zikikaribia, mastaa kibao wa soka watataka kwenda kuandika majina yao kwenye vitabu vya kihistoria vya mchezo huo.

6.Paulo Dybala –Argentina
Muargentina huyo tayari ameshabeba mioyo ya mashabiki wa Juventus kilichobaki ni kwa timu yake ya taifa tu, Argentina. Kikosi hicho cha Amerika Kusini bila ya shaka kitahitaji shujaa mwingine nje ya Lionel Messi kuwafanya kwenda kutamba kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika huko Russia baadaye mwaka huu. Kitu kilichopo ni kama kocha atamchagua staa huyo kumjumuisha kwenye kikosi chake kwa ajili ya fainali hizo kwa sababu ni staa anayesubiriwa kwa hamu kwenye michuano hiyo kuona kile anachoweza kwenda kukifanya.

5.Kylian Mbappe –Ufaransa
Huko Ufaransa, Kylian Mbappe hana alichobakiza soka lake limemfanya kuwa kipenzi cha mashabiki wa mchezo huo katika ligi ya huko. Amekuwa akipata namba mbili katika kikosi cha timu ya taifa ya Les Bleus. Msimu uliopita, mshambuliaji huyo kinda alifunga mabao sita kwenye Ligi ya Mabingwa na kuisaidia AS Monaco kufika nusu fainali kwa mara yao ya kwanza tangu mwaka 2004. Kwa sasa yupo kwenye kikosi cha Paris Saint-Germain. Wakati Les Bleus ikiwa kiwanda cha kufyatua mastaa wenye vipaji, Mbappe ni mmoja wa wachezaji wanaotazamwa kwenda kung'ara katika fainali hizo za Russia kuthibitisha uwezo wake kwenye mchezo huo.

4. Gabriel Jesus –Brazil
Linapokuja soka la kimataifa ni ngumu kuamini kwamba kuna mchezaji kinda ambaye ni muhimu kwa taifa lake kuliko illivyo kwa Gabriel Jesus huko Brazil. Kile ambacho Gabriel  alikifanya kwenye mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Brazil hakuna mashaka na kinamfanya awe na uhakika wa kupata nafasi labda kama tu atakuwa mgonjwa. Licha ya ndoto zake za kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kuzimwa na Liverpool msimu huu, staa huyo wa Man City anasubiri huko Russia kwenda kuing'aricha Brazil kama ilivyokuwa enzi za shujaa wake, Ronaldo Nazario.

3. Leroy Sane –Ujerumani
Ujerumani, siku zote ni moja ya timu zinazopewa nafasi kubwa ya kwenda kubeba ubingwa wa michuano ya Kombe la Dunia inapofanyika. Sane ni mmoja wa wachezaji wanaofanya vizuri kweli kweli kwenye kikosi chake huko Manchester City jambo ambalo hutarajii kumwona nje ya kikosi cha Ujerumani kitakachokwenda kwenye fainali hizo za Russia. Sane ni moja ya mawinga ambao mashabiki wanawasubiri kwa hamu kwenda kuona kile watakachokifanya kwenye fainali hizo za Russia.

2. Raheem Sterling –England
Sterling anacheza soka la kiwango chake msimu huu huko kwenye kikosi cha Manchester City katika Ligi Kuu England. Huwezi kuona England ikifanya makosa ya kushindwa kulijumuisha jina lake kwenye kikosi chao kama ataendelea kuwa fiti hadi mwisho wa msimu bila ya kusumbuliwa na majeruhi yoyote. Sterling ni moja ya wachezaji ambao mashabiki wa England watakuwa wanatumaini mambo makubwa kutoka kwake hasa katika kipindi hiki ambacho wakali wao wengine wa maana kama Wayne Rooney hatakuwapo katika fainali hizo za Russia 2018.

1.Romelu Lukaku –Ubelgiji
Huko Mancheester United, Romelu Lukaku ameaminika na kocha Jose Mourinho na kuwa chaguo la kwanza kwenye nafasi ya ushambuliaji, ambapo kwa msimu huu panga pangua amekuwa hakosi katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo yenye maskani yake Old Trafford. Siku za karibuni, Lukaku pia amefanikiwa kuonyesha kiwango bora kabisa kwenye kikosi chake huku Ubelgiji wakifirahia jambo hilo kwa sababu fowadi wao anakuwa fomu katika kipindi mwafaka, fainali za Kombe la Dunia zikikaribia kabisa. Lukaku ni mmoja wa wachezaji ambao wanatazamiwa kwenda kuandika majina yao kwenye vitabu vya kihistoria katika fainali hizo zitakazofanyika huko Russia.