#WC2018:Mkwanja wa waamuzi Russia kufuru

Muktasari:

Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) limetangaza majina ya waamizu 36 na waamuzi wasaidizi 63 ambao, watachezesha kuanzia hatua ya makundi hadi fainali ila hiyo mishahara yao na posho temea mate chini mwanangu.

HUKU kwenye soka la Bongo wanaonekana wazushi tu, lakini katika fainali za Kombe la Dunia 2018 waamuzi hawashikiki aisee.
Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) limetangaza majina ya waamizu 36 na waamuzi wasaidizi 63 ambao, watachezesha kuanzia hatua ya makundi hadi fainali ila hiyo mishahara yao na posho temea mate chini mwanangu.
Iko hivi. Waamuzi hao wamepangwa kwenye madaraja tofauti lakini ishu kubwa ni hiyo mishahara kwani, kuna waamuzi watakuwa wakilipwa Euro 57,000 (Sh91 milioni) na posho ya Euro 2500 (Sh4 milioni) kwa mashindano, mkwanja ambao unaweza kuwasajili mastraika matata wenye sifa na viwango kama Emmanuel Okwi, John Bocco ama Obrey Chirwa wanne.
Kwa mujibu wa jarida la UOL Esporte la Brazil, limeandika kuwa Fifa wametenga waamuzi hao kwenye madaraja tofauti kulingana na rekodi na uzoefu. Baadhi ya waamuzi ambao watalipwa pesa ndefu ni Felix Brych (Ujerumani), Cuneyt Cakir (Uturuki) na Nestor Pitana (Argentina) ambao watavuna Euro 57,000 na posho ya Euro 2,500 kwa mechi watakazochezesha.
Waamuzi wasaidizi watalipwa Euro 20,000 na posho ya Euro 1,600 kwa kila mechi.