#WC2018:Messi gumzo kila kona unaambiwa!

Muktasari:

Messi huyu hajawahi kushinda Kombe la Dunia na sasa anatua Russia akiwa na Argentina yake ambayo imekuwa akiibeba mabegani licha ya kuwa na mastaa kibao kikosini.

KILA shabiki wa soka duniani anakubali kuwa kwa sasa kuna mfalme mmoja tu, Lionel Messi. Ameshinda kila kitu ngazi ya klabu na ameandika rekodi kibao tamu ambazo itachukua miaka kadhaa kuja kuvunjwa, lakini kuna kitu kinakosekana kwenye kabati lake la medali kule kijijini Rosario.
Messi huyu hajawahi kushinda Kombe la Dunia na sasa anatua Russia akiwa na Argentina yake ambayo imekuwa akiibeba mabegani licha ya kuwa na mastaa kibao kikosini.
Hilo limemsukuma staa wa zamani wa Argentina, Carlos Bilado ambaye alikuwapo kwenye kikosi cha nchi hiyo kilichobeba taji la dunia mwaka 1986.
“Messi (Lionel) kwa hakika atakumbukwa kwa kuwa miongoni mwa wachezaji bora kuwahi kutokea duniani, lakini bado ana kazi ya kutengeneza historia kama ilivyokuwa kwa Pele na Maradona, anatakiwa kushinda taji la Kombe la Dunia,” alisema Bilado, ambaye kwa sasa ni kocha.
Kwa muda mrefu sasa Messi amekuwa akipambana kusaka taji hilo, ambapo mwaka 2014 aliiwezesha Argentina kufika fainali za Kombe la Dunia pamoja na fainali tatu za Copa America (mwaka 2014, 2015, na 2016) lakini hakuna taji alilobeba kwa kuwa zote alipoteza.
Kwa Bilado hilo ni doa kubwa kwa Messi katika kuboresha rekodi zake na kwamba, kama atashindwa kubeba taji la dunia, ufalme wake unaweza kuendelea kuhojiwa na wapenda soka.
“Siku zote Messi analinganishwa na Maradona, lakini ili aweze kukaa kwenye daraja hilo ni muhimu akabeba taji la duniani kwa ajili ya Argentina. Mashabiki wanatamani kuona Messi amenyanyua taji hilo ili kukamilisha cheo chake kwenye ulimwengu wa soka,” alifunguka.
Katika fainali hizi zinazofanyika kule Russia, Messi na Argentina yake ni miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kubeba taji hilo.