#WC2018: KIBOPA: Kutana na mwamuzi milionea anayetamba Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Hata hivyo, safari hii wamekutana na mwamuzi ambaye naye ana pesa kama wao.

DAWA ya jeuri kiburi. Wachezaji wengi mastaa wanaotamba Kombe la Dunia kule Russia wanajisikia sana kutokana na umaarufu wao lakini pia kutokana na jeuri ya pesa.

Hata hivyo, safari hii wamekutana na mwamuzi ambaye naye ana pesa kama wao.

Bjorn Kuipers, mwamuzi wa kimataifa wa Uholanzi ambaye alichezesha pambano kati ya England na Sweden ambalo liliiona England ikitinga nusu fainali, ni mwamuzi milionea zaidi katika michuano ya Kombe la Dunia.

Kuipers, 45, anaweza kuwa tajiri zaidi kuliko baadhi ya wachezaji anaowachezesha kutokana na kuwa mmiliki wa Supermarket nyingi kwao Uholanzi zinazojulikana kama Jumbo Supermarkets ambazo zimezagaa karibu nchi nzima.

Kuipers aliyezaliwa katika Mji wa Oldenzaal, Uholanzi alisoma masomo ya biashara akiwa katika chuo kikuu na mwaka 2016 utajiri wake ulikuwa unakadiriwa kufikia kiasi cha Pauni 11.5 milioni huku akitengeneza faida ya Pauni 2 hadi 3 milioni kwa mwaka.

Kuipers ameripotiwa kuingiza pia pesa ya kutosha katika kazi yake ya uamuzi na ni nadra kwake kujilipa kutokana na faida anayotengeneza katika maduka yake. Alijikita katika uamuzi kwa sababu baba yake pia alikuwa mwamuzi wa soka ingawa ni wa ridhaa.

Biashara yake imekuwa ikimuingizia pesa nyingi kiasi cha kwamba amekuwa mdhamini wa dereva maarufu wa mbio za Formula One, Max Verstappen, ambaye anaendesha kupitia Timu ya Red Bulla na Jumapili katika mbio nza Austrian Grand Prix alivaa kofia ngumu ya chuma yenye rangi za njano ambayo ni nembo ya Jumbo.

Katika fainali za Kombe la Dunia mwaka huu, Fifa imechagua waamuzi 36 kwa ajili ya michuano hiyo na kila mwamuzi amepokea kiasi cha Dola 70,000 kama malipo ya kuwepo kwake katika michuano hiyo. Hata hivyo, kwa mechi mwamuzi anapokea Dola 3,000.

Waamuzi wasaidizi maarufu kama washika vibendera wanalipwa kiasi kiasi cha Dola 25,000 kama malipo ya uwepo wao Russia wakati kila mechi wanapewa kiasi cha Dola 2,5000.

Kuipers mekuwa katika orodha ya waamuzi wa Fifa tangu mwaka 2009 huku akiwa mwamuzi wa juu wa Uefa tangu mwaka 2009. Alichezesha katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Brazil na ingawa katika fainali hizi amekuwa na bahati lakini katika fainali zilizopita alishika filimbi wakati England ikichapwa na Italia.

Tayari Kuipers ameshaonyeshana kiburi na mastaa mbalimbali ambao walijaribu kumsumbua katika michuano hii. Katika pambano kati ya Brazil dhidi ya Costa Rica hatua ya makundi alisikika akimwambia staa wa Brazil, Neymar ‘Funga mdomo wako’ baada ya staa huyo kuanza kulalamia maamuzi yake.

Kuipers alikuwa amebadilisha maamuzi yake ya awali ya kuizawadia Brazil penalti baada ya Neymar kujiangusha lakini akapata msaada wa marudio ya video na ndipo alipobadilisha maamuzi yake huku Neymar akiendelea kulalamika.

Katika pambano kati ya England na Sweden, mwamuzi huyo alimkaripia kiungo wa England, Jordan Henderson ambaye alikuwa amelalamikia vikali maamuzi yake ya kuruhusu wachezaji wa Sweden kuzuia mpira alioupiga haraka haraka.

Hata hivyo, Kuipers aliingia lawama mitandaoni wakati alipochezesha pambano la mtoano kati ya Russia dhidi ya mabingwa wa zamani Hispania ambapo wenyeji walifanikiwa kusonga mbele kwa kutumia mikwaju ya penalti.

Alishutumiwa kwa kejeli mitandaoni kwamba alikuwa anaendeshwa na Rais wa Russia, Vladimir Putin kutokana na maamuzi yake ambayo yalionekana kuinufaisha zaidi Russia. Moja kati ya maamuzi hayo ilikuwa ni penalti aliyowapa wenyeji baada ya Gerrard Pique kuuzuia mpira wa kichwa wa mshambuliaji, Artem Dzyuba kwa mkono ingawa Pique alikuwa anatazama mwelekeo tofauti na mpira.

Kuipers ni mmoja kati ya waamuzi wenye majina makubwa barani Ulaya na amekuwa akiaminiwa na Uefa. Alikuwa mwamuzi wa kati katika pambano la fainali Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kati ya Barcelona dhidi ya Juventus mwaka 2014.

Mei mwaka huu, alikuwa mwamuzi katika pambano la Michuano ya Europa kati ya Atletico Madrid dhidi ya Marseille na kumekuwa na hisia kwamba huenda akapewa pambano la fainali Kombe la Dunia mwaka huu.

Kuiper alikuwa mwamuzi wakati Timu ya Taifa ya England chini ya umri wa miaka 20 ikichukua ubingwa kwa kuichapa Venezuela bao 1-0 katika michuano ya chini ya umri huo iliyofanyika Korea Kusini mwaka jana.