Kiungo aipotezea Yanga SC

YANGA inaendelea kutikisa taratibu kwenye usajili ambapo Ofisa Habari wake, Dismas Ten, hivi karibuni aliweka kwenye mtandao picha ya kiungo wa Rayon Sports, Pierre Kwizera, lakini nyota huyo ni kama vile amewapotezea kimtindo.

Pamoja na Yanga kuweka hadharani nia ya kumtaka, nyota huyo wa zamani wa Simba, mchezaji mwenyewe amesema hajazungumza na yeyote kutoka timu hiyo.

“Namaliza mkataba mwishoni mwa mwezi huu, lakini bado sijaongea na mtu yeyote kutoka Yanga mpaka hivi sasa,” alisema mchezaji huyo kwa kifupi.

Yanga inahaha kujiimarisha kuelekea kwenye mechi zijazo za Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi Kuu Bara msimu ujao, lakini mpaka sasa hakuna mchezaji hata mmoja amesaini ambapo tatizo kubwa linalotajwa klabuni hapo ni ukata.