#WC2018: Huyu jamaa anaishi kistaa kisa kafanana na Mohamed Salah

Muktasari:

  • Kitu kizuri ni kwamba Hussein Ali naye ni mwanasoka, lakini si wa kiwango kikubwa kama alichonacho Mo Salah, hivyo kitu ambacho kimemfanya kuwa maarufu ni kufanana kwake tu na supastaa huyo wa Liverpool na Misri.

LONDON, ENGLAND. KWANI unataka kufanana na nani? Yule aliyefanana na Mohamed Salah anaishi kistaa huko Iraq kuliko hata anavyoishi Salah mwenyewe.

Kitu kizuri ni kwamba Hussein Ali naye ni mwanasoka, lakini si wa kiwango kikubwa kama alichonacho Mo Salah, hivyo kitu ambacho kimemfanya kuwa maarufu ni kufanana kwake tu na supastaa huyo wa Liverpool na Misri.

Ali amekuwa akiombwa kupiga selfie na mashabiki kila anapokatiza na kali zaidi alikwenda hadi kwenye ile fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyofanyika Ukraine.

Alivyo Ali ni kama vile kopi ya Mo Salah, kwa sababu wawili hao wamefanana kwelikweli mithiri ya pacha.

Kwa sasa, Ali anacheza katika kikosi cha Al Zawraa akiwa mshambuliaji na mwenyewe anadai ndoto zake ni kucheza soka la kiwango cha juu na kumfikia mtu ambaye kwa sasa amemfanya kuwa maarufu zaidi.

Alisema: “Tunacheza nafasi moja na nitafanya kila kitu kukopi kile anachofanya hadi utembeaji wake. Anasoma Kuran na kuomba dua kabla ya mechi. Nami pia nasoma kuran na kuomba dua pia.”

Katika kufanana kila kitu na Mo Salah, Ali ameamua hata kununua jezi za Liverpool, ambapo wakati mwingine anapozitupia, imekuwa ikiwaweka mashabiki wa soka katika wakati mgumu kutambua kama huyo ni Salah halisi au Salah feki.

Wakati mwingine hata mashabiki wamekuwa wakifikia hatua ya kumwambia apone haraka maumivu yake ya bega aliyoumia kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati yeye si mchezaji husika.

“Nilipokwenda kucheza mechi dhidi ya Al Ahed, watu walikuja kupiga picha na mimi, kila ninapokatiza, watu wamekuwa wakiomba kupiga picha na mimi, hata wanawake pia!” alisema Ali.

“Mohamed Salah alipoumia, watu kibao walikuja kwangu na wengine kuniambia nipone haraka wakidhani mimi ndiye yeye.”