#WC2018:Huyu Isco atalaza watu na viatu

Muktasari:

Kuna nyota ya mchezaji mmoja katika kikosi cha La Roja inakwenda kung’ara pasi na maelezo katika fainali za Kombe la Dunia huko Russia.

AMA kweli kila nabii na zama zake.
Kuna nyota ya mchezaji mmoja katika kikosi cha La Roja inakwenda kung’ara pasi na maelezo katika fainali za Kombe la Dunia huko Russia.
Achana na kichaa Sergio Ramos aliyekunywa maji ya bendera ya Hispania, fanya kama unamsahau kiungo mkongwe Andres Iniesta anayezeeka na udambwi udambwi wake, huyu nyota alishatabiriwa kufanya vyema hata na kipa wa kikosi hicho, David De Gea muweke pembeni, kuna mtu anaitwa Isco, ni balaa la mwaka.
Wazazi wake walimpomzaa, wakamwita jina la Francisco Roman Alarcon Suarez, lakini kupunguza maumivu mabaya ya pumzi na kupunguza muda pia, kwenye soka anafahamika kwa jina lenye herufi nne tu, Isco.
Asikwambie mtu, huyu jamaa ni fundi haijawahi kutokea. Pale kwenye kikosi cha Real Madrid yale mambo anayoyafanya, hakika akienda kwa moto huo huo huko kwenye fainali za Kombe la Dunia, basi wapinzani watakaoikabili Hispania watakuwa kwenye matatizo makubwa.
Isco si mchezaji anayeishi sana kwa kiki, hazungumzwi sana lakini mambo yake yeye anayaonyesha ndani ya uwanja. Katika fainali hizo kama La Roja watamwaamini na kutumia kikosi cha wachezaji vijana wakiwamo Marco Asensio, Iago Aspas, Alvaro Morata, Thiago Alcantara, Jordi Alba, De Gea, David Silva basi mashabiki watakwenda kushuhudia soka lililojaa uhondo mkubwa.
Isco ni kawaida yake anapokuwa uwanjani basi kuutaka mpira muda wote. Argentina wanamfahamu vizuri baada ya kuwapiga hat-trick katika mechi ya kirafiki, ambapo timu hiyo ya Lionel Messi ilichapwa 6-1.
Messi hakucheza mechi hiyo, lakini aliishia kumtazama tu mpinzani wake huyo wa kwenye El Clasico akifanya mambo yake ndani ya uwanja.
Isco ameichezea Hispania mara 26 tu, lakini tayari ameshatikisa nyavu mara 10 jambo linaloonyesha kwamba ni staa wa kutisha anapokuwa ndani ya uzi wa La Roja.
Kwa silaha hiyo ya Isco pamoja na ya mastaa wenye uchu wa kushinda kama Diego Costa, inaonekana wazi kabisa kwamba Hispania watakwenda kwenye fainali hizo za Russia kivingine kabisa, kwenda kurudisha utawala wao wa soka wa miaka ya 2010, walipobeba taji hilo lilipofanyika kwa mara ya kwanza kwenye ardhi ya Bara la Afrika huko Afrika Kusini.