He! Lionel Messi, Paul Pogba acha katambe

EL Clasico inapigwa huko Russia. Lionel Messi wa Barcelona ataumana jino kwa jino la Luka Modric wa Real Madrid. Hii itakuwa kwenye fainali za Kombe la Dunia.

Ambaye ametajwa mwanzo atakuwa na kikosi chake cha Argentina, wakati mwingine atakuwa upande wa Croatia. Kwenye hiyo El Clasico ya Russia, Ivan Rakitic, atamsaliti Messi na kwenda upande wa Modric. Hili ni bonge la mechi.

Linarudisha ule ushindani wa Barca na Real Madrid. Mechi hiyo pia itakuwa ya upinzani wa Liverpool na Manchester United, kutokana na uwepo wa Dejan Lovren, mkali wa Anfield atakayekuwa na Croatia, wakati Marcos Rojo wa Old Trafford atakuwa upande wa Argentina. Kuna upinzani pia wa Inter Milan na Juventus ambapo Ivan Perisic wa Inter atakuwa na Croatia na Gonzalo Higuain na mwenzake Paulo Dybala wa Juventus watakuwa upande wa Argentina. Kuna Mario Mandzukic pia, ambaye kwenye mechi hiyo ya leo ataweka kando urafiki na kina Dybala na Higuain kwa sababu wanacheza timu moja, Juventus huko Italia.

Utamu wa mechi hiyo ni kwamba, Messi na chama lake la Argentina atahitaji kupata ushindi ili kuweka hai matumaini ya kusonga raundi inayofuata baada ya kubanwa mbavu kwenye mechi ya kwanza walipotoka sare dhidi ya Iceland.

Croatia wao walishinda mechi yao ya kwanza kwa Nigeria, hivyo hata wakitoka sare watakuwa wamejiweka pazuri, licha ya kwamba ushindi utakuwa umewahakikishia zaidi nafasi ya kutinga hatua inayofuata. Hicho ndicho kinachofanya mechi hiyo kuwa na mvuto wa kipekee.

Mechi nyingine zitakazopigwa leo, Alhamisi, Denmark wenye supastaa matata kabisa Christian Eriksen watakuwa na kibarua mbele ya Australia, wakati Ufaransa watakuwa na kasheshe kwa kumenyana na Peru. Hii ni mechi ya Kundi C.

Ufaransa yenye mastaa wengi akiwamo Paul Pogba itahitaji kushinda mechi hiyo kutinga hatua inayofuata, sawa na ilivyo kwa Denmark, ambapo pia itataka ishinde ili kufunga hesabu mapema kabla ya kukutana wenyewe kwa wenyewe kwenye mechi ya mwisho.

Kwenye kundi hilo, Ufaransa na Denmark kila moja imejikusanyia pointi tatu, hivyo wamekuwa na nafasi nzuri labla kama tu kutakuwa na mabadiliko yatakayofanya upepo kwenye kundi hilo kubadilika. Shughuli nzito kwa mechi za leo iko kwa Messi, ambaye atakuwa na uamuzi wa kuhusu hatima ya timu yake katika fainali hizo, ambazo miaka minne iliyopita wakikwama kwenye mechi ya fainali baada ya kuchapwa na Ujerumani huko Brazil. Messi atafanya maajabu?