#WC2018:Chimbo la Uruguay na Misri hili hapa

Muktasari:

  • Mechi hii inatarajiwa kuwa na mvuto wa hali ya juu kutokana na kukutanisha mastaa wanaofanya vizuri kwenye soka kwa sasa barani Ulaya. Timu hizi ambazo zipo kundi A sambamba na wenyeji wa mshindano hayo zimeshachagua mahali ambapo zitaweka kambi zao.

Timu ya taifa ya Uruguay na Misri zinatarajiwa kuumana kwenye mechi ya hatua ya makundi ya Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu, katika mechi itakayopigwa Juni 15 kwenye dimba la Ekaterinburg Arena nchini Russia.

Mechi hii inatarajiwa kuwa na mvuto wa hali ya juu kutokana na kukutanisha mastaa wanaofanya vizuri kwenye soka kwa sasa barani Ulaya. Timu hizi ambazo zipo kundi A sambamba na wenyeji wa mshindano hayo zimeshachagua mahali ambapo zitaweka kambi zao.

Sehemu hizi ndiyo watazitumia kwa ajili ya malazi, mazoezi na maandalizi ya michezo yao mpaka watakapoondoka nchini Russia. Sehemu ambazo timu hizo zitafikia ni:

Misri (Grozny Hotel, Chechnya)

Wawakilishi hawa wa bara la Afrika ambao wamefuzu fainali hizi baada ya miaka 28 wataweka kambi eneo la Chechnya kwenye Hoteli mpya ya Grozny. Hoteli hii ilijengwa maalum kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia 2018.

Grozny hotel ipo karibu kabisa na Uwanja wa Akhmat Arena, ambao timu hiyo itautumia kwa ajili ya mazoezi kipindi chote cha mashindano. Uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 30,000 unamilikiwa na timu ya eneo la Chechnya inayoitwa FC Akhmat.

Uwanja huo una viwango vyote vinavyohitajika kwa wachezaji kufanyia mazoezi. Kwa hivi sasa, timu ya taifa ya Russia inautumia uwanja huo kwa ajili ya kufanyia mazoezi ya kujiandaa na mechi mbalimbali za kimataifa.

Uruguay (Borskiy Sports Centre, Nizhny Novgorod)

Luis Suarez na wenzie wa timu ya taifa ya Uruguay wamechagua kuweka kambi kwenye kituo cha michezo cha Borskiy kilichopo Bor kwenye mji wa Nizhny Novgorod. Eneo hilo ni moja ya maeneo rafiki kwenye mji wa Nizhny Novgorod kutokana na kusheheni miundombinu ya usafiri.

Kituo hicho ambacho Uruguay wataweka kambi yao, kimejengwa maalum kwa ajili ya matumizi ya Fainali za Kombe la Dunia 2018. Kituo hicho kina Hotel kubwa yenye vyumba 75, sehemu ya matibabu, eneo la mazoezi ya viungo (Gym) pamoja na uwanja wa kufanyia mazoezi.