#WC2018: Cheki hii hapa, dakika 90 tu Sh850 bil

Muktasari:

  • Sasa habari hii iko huko Russia. Kuna wanaume watapewa fedha hizo leo baada ya fainali ya Kombe la Dunia. Bingwa anapata fedha hizo na Kombe lililonakshiwa kwa dhahabu.

Hebu wewe msomaji fikiria, kwa mfano leo hii unapewa Sh852 bilioni kwamba hizo ni fedha zako tu, labda umeshinda bahati nasibu, unaweza ukapata presha au unaweza kuzimia au vyovyote vile. Utaona ni ushindi wa aina yake.
Sasa habari hii iko huko Russia. Kuna wanaume watapewa fedha hizo leo baada ya fainali ya Kombe la Dunia. Bingwa anapata fedha hizo na Kombe lililonakshiwa kwa dhahabu.
Fifa imetangaza mzigo huo wa maana kwa bingwa wa mwaka huu. Mwanzoni bingwa alikuwa akilamba Dola358 milioni na kombe na mara ya mwisho zilichukuliwa na Ujerumani mwaka 2014 katika fainali za Rio de Janeiro, lakini bingwa wa mwaka huu, atalamba Dola400 milioni (Sh852bilioni fedha za Tanzania).
 
Usione hivi, timu zilipigana vikumbo Kombe la Dunia, mambo yake ni makubwa. Timu zilipambana kwa ajili ya mengi. Kwanza kabisa heshima, pili rekodi lakini tatu ni fedha. Fifa inataka kuona watu wa mpira wanafurahia kazi yao na zaidi ni kuifanya soka ichangamkiwe.
Kuongezeka kwa fedha hizo, shughuli nzima imefanywa na Gianni Infantino, Rais wa Fifa ambaye amefanya maboresho mengi katika kila mashindano yanayosimamiwa na Fifa.
Ukiacha hiyo ya rekodi na heshima, na tambo za kumfunga mwingine, hakuna tena kama mzigo wa fedha ambao timu bingwa zinazawadiwa.
Katika mashindano mbalimbali, timu zinapotolewa ndiyo shughuli yako imemalizika, lakini kwa Fifa iko tofauti. Hata anayefanya vibaya ana fungu lake.
Iko hivi, timu 16 zilizotolewa kwenye hatua ya makundi, kila mmoja amelamba Dola8 million wakati timu nane zilizotolewa hatua ya 16 Bora zilipozwa na Dola12 milioni kila mmoja.
Timu zilizotolewa kwenye robo fainali zililamba Dola16 milioni kila mmoja. Timu iliyoshika nafasi ya nne ambayo ni England imeondoka na Dola 22 milioni. Mshindi wa tatu ambaye ni Ubelgiji ilipata Dola24 milioni. Mshindi wa pili Dola28 milioni na bingwa atapata Dola38 milioni.
Mbali na fedha hizo, Fifa ilitanguliza fedha za maandalizi kwa timu zote 32 kuwa kila mmoja alipata Dola1.5 milioni.
Fifa pia ilianzisha mpango maalumu wa kusaidia klabu, kwamba zimetengwa Dola209 milioni kama bonasi kwa ajili ya klabu zilizoruhusu wachezaji wake kucheza Kombe la Dunia.
Pia Fifa imetenga Dola134 milioni kama fedha za kinga au bima kwa ajili ya fidia kwa wachezaji kwa klabu ambazo wachezaji wake watapata majeraha wakiyatumikia mataifa yao. Kwa fainali za mwaka huu, Fifa imeongeza Dola791 milioni ikiwa ni asilimia 40 zaidi ya fedha zilizotolewa fainali zilizopita.